Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha wa Fei Toto anusurika kufa mechi ya Yanga

Kocha Fei N Kocha wa Fei Toto anusurika kufa mechi ya Yanga

Sat, 4 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ukiona changamoto zinakukatisha tamaa kwenye ndoto zako, jifunze kwa wengine waliopambana nazo na sasa wanaelekea kutimiza malengo yao na wengine wanaishi kwenye matamanio yao.

Kocha wa timu za vijana za Zanzibar, Mohamed Mulishona 'Xavi' (34) pia anafundisha Magnet Yourth Sport Academy na wachezaji binafsi akiwemo Feisal Salum 'Fei Toto' anasimulia visa na mikasa aliyokutana nayo kwenye maisha yake.

Kocha huyo mwenye tabasamu mwanana na msikivu anapoulizwa jambo, wakati anafunguka mapito yake sura yake ilibadilika kidogo ilionyesha huzuni inayoashiria makovu ya maumivu yaliobakia moyoni mwake.

Pamoja na hilo, kinywa chake kinakiri ushindi na kutamka mipango mikubwa aliyonayo kwenye soka na anataka awe mfano wa kuigwa na wengi.

"Nimejifunza kuamini Mungu akitaka unapata asipotaka hupati, haijalishi mapito gani utakumbana nayo kwenye utafutaji, unayeniona hivi sikutarajia ningekaa sawa kulingana na magumu niliyokutana nayo," anasema.

2010 HATAISAHAU Wiki moja kabla ya kufanya mtihani wa kidato cha sita katika Sekondari ya Haile Salasie, Xavi alikumbwa na tatizo lililozima ndoto zake za elimu ambapo alitamani kusomea udaktari.

"Nilikuwa darasani nilianguka ghafla baada ya kurudishwa nyumbani macho yakapofuka nikawa sioni kabisa ndani ya miezi tisa,jambo lililopelekea nisifanye mitihani na nilikuwa na akili sana namba zangu kwenye mtihani ilikuwa ni ya kwanza na pili;

"Wazazi wangu walipambana kadiri wawezavyo wakanitibia tatizo la macho nikaanza kuona, likaja tatizo lingine la kushikwa na wazimu ndani ya miaka mitano na yote hayo yalikuwa yanakuja nikijaribu kurejea darasani, ila nikikaa tu bila kazi yoyote nakuwa mzima kabisa, nikaamua kuachana na mambo ya shule ili kuyanusuru maisha yangu.

Anaendelea kusimulia kuwa; "Kwenye soka nako nikakumbana na mitihani mingine iliyotaka kuyaondoa maisha yangu duniani, ilikuwa 2014 tulicheza dhidi ya Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi, kuna mchezaji alinikanyaka tumboni nikachanika chango, nikakimbizwa hospitali ambako nilishonwa hadi leo nina alama kubwa inayoonyesha jeraha hilo.'

"Baada ya kupona nikajaribu tena  kurudi uwanjani nilikuwa nachezea Jang'ombe, kuna mechi nilichezewa rafu hadi nikazimia, nikaona nisije nikapoteza maisha yangu nikaachana na mpira, hilo linanifanya niwe na uchungu wa kuhakikisha wanaopata nafasi ya kucheza nawasaidia kufika mbali."

Xavi ambaye ni baba wa mtoto mmoja anayeitwa Iqram (5), anasema jaribu la kwenye elimu na uwanjani, ndio sababu ya kusomea ukocha, jambo ambalo linafanikiwa. "Hatua niliyopo ya kusoma ni Diploma A ya Caf, ambapo mwezi ujao nitarudi darasani na awamu hii kituo kitakuwa Tanga ni kozi inayochukua mwaka mzima, ndio maana tunapewa muda wa kufundisha."

KUFUNDISHA WACHEZAJI BINAFSI Anasema kwenye nchi zilizoendelea ni jambo la kawaida kocha ama mchezaji kufanya mazoezi binafsi kwa ajili ya kurekebisha madhaifu yake.

"Tena mazoezi hayo yanahitajika zaidi kwa Afrika, Ulaya ambako ndiko wanafanya zaidi bado mabenchi yao ya ufundi yana makocha wa washambuliaji, mabeki, viungo na makipa,hapa kwetu sana sana utakuta wa makipa, viungo na kocha mkuu, hivyo inakuwa ngumu kwa mchezaji kubadili madhaifu yake.

Anataja faida za mazoezi binafsi kuwa; "Ninaowafundisha mimi nimewatazama kwenye mechi zao, nimeona madhaifu ninayoyafanyia kazi na baada ya hapa nitawaangalia tena kama wamebadilika, ili waendane na soka la kisasa wanahitaji kujifunza zaidi.

"Mfano Christiano Ronaldo anaonekana ana vitu vya tofauti uwanjani ni kati ya mastaa walio na mazoezi binafsi licha ya ligi zao kuwa na makocha wa kila aina kwenye benchi ambao ni rahisi kuwaelekeza."

MASTAA WA LIGI KUU Kuna wachezaji mbalimbali anaowafundisha mazoezi binafsi pindi wanapopata mapumziko ama Ligi Kuu inapomalizika anawataja ni Abdallah Shaibu 'Ninja' (Yanga), Chrispin Ngushi (Yanga), Amina Ramadhan (Simba Queens), Ibrahim Bacca (Yanga), kipa Ahmed Salula (alikuwa Azam), Mohamed Mmanga (Polisi Tanzania), Abdul Aziz Makame (Kagera Sugar), Ibrahim Abdallah (Namungo).

Wakati Feisal Salum 'Fei Toto' anapokuwa Zanzibar basi anampa mazoezi maalumu kipindi ambacho yupo nje na timu, akishughulikia changamoto zake, alifanya hivyo na kwa Mudathir Yahaya kabla hajasaini Yanga.

"Hao ni kwa upande wa Bara wapo na wengine wanaotoka sehemu mbalimbali, pia wapo walioweka oda mfano Mudathir pindi Yanga itakaporejea atakuwa anakuja, kuna Hassan Kessy, ninachokifanya ni kawaida kwa nje mastaa huwa wanawafuata makocha binafsi ili kujiweka kwenye ushindani," anasema.

Kuhusu akademi anasema malengo ni kuwaandaa vijana wa kwenda kuwauza nje na Ahmed Bakari 'Pipimo' anatarajia kwenda Celta Vigo ya Hispania kufanya majaribio kwa muda wa miezi mitatu.

"Nina vijana wadogo wana miaka 15, 16 na 17 tunawaandalia misingi ambayo wakienda nje hawatakutana na changamoto, ambazo zinawasumbua kaka zao wanaokwenda nje na kushindwa kupata nafasi za kucheza kutokana na kutolelewa kwenye misingi sahihi  ya soka," anasema.

KAYUNI, MIRAMBO Anasema kozi za ukocha zinawafumbua macho, anaamini kuna vitu vinakwenda kubadilika kwenye soka la Tanzania na kumuomba Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Oscar Mirambo na Mkufunzi Sunday Kayuni kuendelea kutilia mkazo makocha kusoma.

"Kabla ya kusoma kozi hiyo tunapewa mifumo ya TFF ambayo lazima tujue Ligi ya Tanzania ni ya aina gani, kwani kila nchi ina soka lake, mfano Zanzibar kuna kila hatua za mchezaji hadi anafikia kupata timu kubwa, hakuna kukurupuka kumuona mchezaji yupo Ligi Kuu ipo misingi yao."

Xavi anasoma kozi hiyo pamoja na Seleman Matola na Juma Kaseja aliowaelezea kuona kitu kwao ambacho kitalifaidisha sola la Tanzania hasa kwa wachezaji wanaotamani kufika mbali.

"Kwanza ni wasikivu, wanapenda kujifunza na yapo mambo ambayo watasaidia kulifanya soka la Tanzania liwe la kisasa zaidi, Kaseja na Matola wamecheza kwa kiwango kikubwa hakuna asijejua," anasema.

Chanzo: Mwanaspoti