Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha mpya Yanga aja na rekodi za Sven

Pic Yangaa Data Kocha mpya Yanga aja na rekodi za Sven

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanaendelea kujifua mazoezini katika kambi yao ya Kigamboni chini ya Kocha Juma Mwambusi, huku wakimsubiria kocha mkuu mpya, Mfaransa Sebastien Migne anayetarajiwa kutua kikosini hapo akiwa na rekodi kama za Sven Vandenbroeck aliyoyafanya Msimbazi.

Ingawa mabosi wa Yanga wamekuwa wagumu kufichua juu ya ujio wa kocha huyo, lakini chanzo makini kutoka ndani ya klabu hiyo, kimeisisitiza Migne anakuja baada ya Hurbert Velud kukomaa kwenye dau la mshahara alioutaka, huku mwenyewe akiteta na gazeti hili kutoka Ufaransa.

Mwanaspoti, linalofahamu Yanga waliamua kumpiga chini Velud kutokana na kung’ang’ania dau kubwa la mshahara, liliwasiliana na Migne jana ili kutaka kujua atakuja lini Tanzania kujiunga na Yanga na Mfaransa huyo alishindwa kukataa au kukubali zaidi ya kushangaa habari zake kuvuja.

“Nyie habari hizi mmezipata wapi...inaonekana basi mnajua mambo mengi juu yangu...haahaahaa,” Migne alijibu kwa ufupi na kuishia kucheka wakati alipotafutwa kwa njia ya whatsapp akiwa kwao Ufaransa, huku akikataa kuweka tarehe ya lini atakuja Tanzania.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha, Mfaransa huyo aliyeipeleka Kenya kwenye fainali za Kombe la Afrika (Afcon 2019), hajawahi kuwa na rekodi kwenye ngazi ya klabu zaidi ya timu za taifa, kama ilivyokuwa kwa Sven ambaye hata hivyo licha ya kudharauiliwa lakini alifanya maajabu mengi Simba.

Simba ilimnasa Sven na kumpa ajira Desemba mwaka juzi, huku baadhi ya mashabiki wakimponda kwa vile CV yake kwenye haikutisha, lakini kocha huyo Mbelgiji aliiongoza Simba kutwaa mataji matatu ndani ya msimu mmoja, huku akiivusha timu hiyo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopo kwa sasa.

Cha kushangaza ni, wakati Sven anatua Simba, Senzo Mazingisa ndiye aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba na safari hii Yanga ikijiandaa kumpokea Migne, Senzo ndiye Mshauri Mkuu wa klabu hiyo, huku Mfaransa huyo pia akiwa hana rekodi tamu katika ngazi ya klabu.

Kwa maana hiyo kama Migne atatua, ni wazi atapaswa kwenda na miujiza aliyoifanya Sven Msimbazi aliyeipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara likiwa ni taji la tatu mfululizo kwao, Kombe la ASFC na Ngao ya Jamii kabla ya kubebwa kwa maafande wa FAR Rabat ya Morocco siku moja tu baada ya kuivusha Simba kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiongoza kwa sasa Kundi A.

Sven alijiunga na Simba akiwa na miaka 40, wakati Migne kwa sasa ana umri wa miaka 48 na rekodi zinaonyesha tangu aanze kuwa kocha mwanzoni mwa miaka ya 2010, amekuwa akitamba zaidi timu za taifa akianza na DR Congo U20 na ile ya wakubwa akiwa msaidizi wa Claude Le Roy kisha Togo, Congo Brazzaville, Kenya na baadaye kutua Guinea ya Ikweta iliyopo kundi moja na Tanzania katika mbio za kuwania Fainali za Afcon 2021 japo waliachana naye mwaka jana.

Mara alipoachana na Guinea ya Ikweta, Migne alijiunga klabu ya Ligue 2 ya Chamois Niort ya kwao Ufaransa na Yanga imepanga kumchukua baada ya kuachana na Hurbet Velud aliyekuwa chaguo la kwanza kwa mabosi wa Jangwani, lakini dau lake la Dola 20,000 za mshahara likiwa kikwazo kwao.

Migne aliyezaliwa Novemba 30, 1972 katika mji wa La Roche-sur-Yon, Ufaransa enzi zake za uchezaji alikipiga katika timu za kwao Ufaransa La Roche VF (1989–1993), Stare de Vallauris (1994–1997) na FC de Gaillard (2000–2002) kabla ya kubukua ukocha na kuanza kufundisha klabu kadhaa kama kocha Msaidizi kabla ya kuanza kupewa timu za taifa kama kocha kamili.

Yanga inahaha kusaka kocha mkuu mpya baada ya kumpiga chini Cedric Kaze aliyeiongoza timu yao kwa siku 142 na kuiacha ikiwa kileleni mwa msimamo na alama zao 50 baada ya mechi 23 mbele ya Simba yenye pointi 46 baada ya mechi 20.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz