Simba SC imepata kocha mpya Robertinho Oliviera raia wa Brazil ambaye alikuwa Visiwani Zanzibar akiishuhudia timu yake ikicheza mechi za Kombe la Mapinduzi ambapo Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu amesema ni mapema sana kocha huyo kutoa tathmini ya wachezaji kwa mechi mbili alizoziona.
Oliviera alishuhudia mechi hizo zilizochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja huku zaidi ya nyota 18 wakikosekana.
Rweyemamu ameyazungumza hayo muda mchache kabla ya timu hiyo kuanza safari ya kurudi Dar es Salaam Ijumaa iliyopita baada ya kuvuliwa ubingwa wa mashindano hayo ikipoteza mechi moja dhidi ya Mlandege bao 1-0 na kushinda bao 1-0 dhidi ya KVZ. Kundi lao Mlandege ndio wametinga nusu fainali ikiwa na pointi nne.
Amesema Simba SC ina wachezaji zaidi ya 20 timu imecheza mechi mbili kocha akiwa jukwaani hivyo ni mapema kwake kutoa tathimini hiyo bali atafanya hivyo baada ya kushuhudia wachezaji wake wote.
“Labda baada ya mchezo wetu na Mbeya City anaweza kuzungumza chochote kuhusu kikosi chake na kuweka wazi nini anakitaka na nini hataki kwasasa ni mapema sana.
“Timu inakwenda Dubai kuendelea na maandalizi ya Ligi kuhusiana na kocha mpya kuanza lini majukumu yake nadhani hilo lipo wazi kuwa anarudi na timu na atakutana na wachezaji wote ili kufanya kikao na baada ya hapo majukumu yake yataanza kama kawaida,” amesema Rweyemamu.