Kuna siri moja Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amewaachia Simba. Kwenye ripoti yake aliyoacha amemwambia Mohammed Dewji ‘Mo’ amng’oe Aziz Ki pale Yanga.
Amekiri kumwambia mchezaji huyo ambaye mkataba wake unaelekea ukingoni Yanga ni mashine na kila alipokuwa akikutana nae alikuwa roho mkononi.
“Nimewaambia wamsajili Aziz Ki wakaniambia watajaribu,” alisema kocha huyo aliyeachana na Simba kiroho safi hivi karibuni huku akisema siku chache kutoka sasa atamalizana na moja ya klabu kubwa ya Afrika.
“Nilimpendekeza Aziz kwa kuwa tayari yuko Tanzania ameshaanza kuzoea mazingira mazuri ni tofauti na mchezaji mpya anayefika kuja kuanza kuzoea mazingira ya hapo,” alifunguka kocha huyo.
Robertinho alisema kama angeambiwa staa mmoja wa haraka kumchukua ndani ya kikosi cha mabingwa hao basi angekuwa Aziz Ki pekee na kama kuna bahati kubwa kwa watani wao ni kuwa na mchezaji bora kama raia huyo wa Burkina Faso.
Kocha huyo aliongeza katika ripoti yake ya awali aliwaomba mabosi wa Simba kumsajilia Aziz Ki ili awe kwa wekundu hao kwa msimu ujao.
“Ni mchezaji bora aliyekamilika kwa kila kitu, wakati mzuri pekee wa Aziz Ki utafurahia akiwa na mpira kama wewe ni timu pinzani na ni pale atakapokuwa eneo la ulinzi lakini sio akiwa kwenye nusu yenu,” alisema Robertinho.
“Yanga wana bahati sana kuwa naye, unapokutana na Yanga lazima ufanye akili ya kuhakikisha hafanyi kazi kwa utulivu wake nafikiri hili ni kosa ambalo wachezaji Simba walilifanya kipindi cha pili tulipokutana nao licha ya kwamba tulikuwa na maandalizi mazuri ya kumzuia.
“Niliwahi kuwaambia viongozi wangu wa Simba kwamba kama wamsajili Aziz Ki utakuwa ni usajili bora sana kwa Simba sijui kama wataendelea na hilo au wataliacha,” kauli hiyo ya Robertinho inakuja wakati ambao mkataba wa Aziz Ki na Yanga unafikia tamati mwisho wa msimu huu nyakati ambazo yuko kwenye kiwango bora kuliko wakati wote tangu alipotua nchini.
Kiungo huyo ni kati ya vinara wa wafungaji akiwa na mabao sdaba sawa na Jean Baleke wa Simba na staa mwenzake wa Yanga, Maxi Nzengeli.
Robertinho alisema kiwango cha Aziz Ki kinawapa ubora mkubwa Yanga na safu yao ya ushambuliaji inakuwa na watu bora wanaojua kufanya maamuzi ya mechi wakati wowote.
“Simba inatakiwa kuendelea kujengwa taratibu, ninachowashauri waendelee kutafuta wachezaji waliobora zaidi, unajua usajili ni kama kamali unaweza kupata wachezaji waliobora lakini wakija kwako wakashindwa kuanza kuonyesha makali kwa kasi.
WAPANIA DIRISHA DOGO
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salum Abdallah ‘Try Again’ amesema wana kila sababu ya kuboresha kikosi chao dirisha dogo la usajili huku akisisitiza watafanya hivyo baada ya ujio wa kocha mpya.
Try Again alifunguka hayo baada ya kuulizwa mpango wao wa usajili dirisha dogo Januari mwakani na alikiri walifanya makosa msimu uliopita dirisha kubwa la usajili hivyo watahitaji kuongeza nguvu.
“Kutengeneza timu sio kazi rahisi na sisi tunahitaji timu ya muda mrefu msimu hii dirisha kubwa tulifanya usajili mkubwa lakini haujaleta mafanikio kama matarajio yetu hivyo nimeongea na mfadhili wetu Mohamed Dewji ‘Mo’ namna ya kuboresha timu nafikiri kuna mambo mazuri yanakuja;
“Umuhimu wa kumuachia kocha ni kuona anasajili wachezaji ambao atawatumia na sio kurudia makosa ya kujaza wachezaji wenye vipaji benchi kwa sababu ya kushindwa kuendana na mfumo ili kukwepa changamnoto hiyo wanamwachia kocha mpya,” alisema.
Alisema wanaweza kusajili mchezaji kutoka Al Ahly akaja Simba akashindwa kucheza kutokana na mfumo w mwalimu kumkataa na sio kwamba hana uwezo hivyo wanasubiri mapendekezo ya kocha wao ajae ili kumpa kile anachokihitaji.
“Kocha ndiye atakayechagua nini anataka tunaelewa dirisha hili sio rahisi kupata wachezaji bora kutokana na wengi kuwa kwenye mikataba ikishindikana watakaopatikana wachache tutafanya linalowezekana na kusubiri dirisha lingine kubwa;
“Wachezaji waliopo Simba ni wazuri na wanavipaji kilichobaki ni kuwa na moyo wa kuipambania timu kama ilivyokuwa kwa Kibu Denis ni mchezaji ambaye akitolewa unaona kabisa timu inavyoyumba.” alisema.
Alisema kipindi cha mwezi mmoja na nusu kilichobaki ni muda wa wachezaji wao wote kupambania timu ili kujihakikishia nafasi ya kubaki kikosini kwani wana mpango wa kuachana na wachezaji ambao hawana wanachokifanya kwaajili ya kuipa timu matokeo.
“Tumetumia gharama kubwa kusajili na tunalipa mishahara wachezaji ambao hakuna wanachokifanya hatutaki wakaa benchi tunataka timu ya wapambanaji hivyo naamini kuna baadhi watatupisha ili tuweze kuingiza watu ambao watatumikia kile tilichowapa.” alisema.
Wakati huo huo, aliwaomba mashabiki na viongozi wa timu hiyo kuungana kwa pamoja wakisahau yaliyopita ili kuirudisha timu kwenye ushindani.
“Tumepokea ushauri na malalamiko ya mashabiki wetu sisi kama viongozi tutafanyia kazi mambo hayo lakini na sisi tunawaomba kurudi tuwe pamoja kwa upendo na ushirikiano ili kuiweka timu kwenye hali nzuri ya ushindani;
“Simba imepoteza kwa mabao 5-1 hili litapita sasa tugeukie kwenye mechi za kimataifa dhidi ya ASEC Mimosas tukiwa na umoja na mshikamano mechi hiyo ndio itakayoturudisha kwenye ushindani,” alisema Try Again.