Wakati Simba ipo Zambia kwa ajili ya mchezo wa hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos, Kocha Mkuu wa Zesco United, George Lwandamina ameipa nafasi ya kushinda.
Akizungumza kutoka Zambia, Lwandamina aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali za Yanga na Azam, alisema mchezo huo hautakuwa mwepesi japokuwa anaipa nafasi kubwa ya kushinda Simba.
“Simba ina wachezaji ambao ni wazoefu zaidi kwenye michuano hii tofauti na Dynamos ingawa jambo kubwa ambalo limekuwa linawabeba ni kucheza kitimu kuliko kumtegemea mchezaji mmoja,” alisema.
Lwandamina aliongeza mabeki wa Simba wanapaswa kuongeza umakini sana pindi watakapokutana na mshambuliaji kinara wa timu ya Dynamos, Andy Boyeli kutokana na kufanya vizuri msimu uliopita.
“Boyeli alisajiliwa akitokea Klabu ya Chambishi na alijiunga nao katikati tu ya msimu uliopita ila aliibuka kinara wa ufungaji bora na kama haitoshi alichukua tuzo ya mchezaji bora wa msimu.”
Raia huyo wa Congo alifunga mabao 18 ambapo akiwa na Chambishi iliyoshuka daraja msimu uliopita akifunga saba na alipohamia Dynamos alifunga 11 hivyo kuibuka kidedea katika Ligi Kuu ya Zambia.
Dynamos ambao ni mabingwa wa Zambia ilifuzu hatua hiyo kwa bao la ugenini baada ya mchezo wa kwanza kupoteza 2-1 dhidi ya African Stars ya Namibia kisha marudiano kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa ikashinda 1-0.
Mchezo wa mwisho kwa timu hizi kukutana ulipigwa Agosti 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika kilele cha Simba Day ambapo Simba ilishinda kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na raia wa Cameroon Leandre Willy Onana na Fabrice Ngoma raia wa DR Congo.