Kwa Yanga, Zlatko Krmpotic, amesema mchezo unaokuja dhidi ya Mbeya City anatarajia kupanga nyota wa kigeni, lengo ni kusaka ushindi utakaorudisha furaha kwa mashabiki.
Mipango hiyo inasukwa na raia huyo wa Serbia baada ya kukiri kuanza vibaya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons kwa kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wake wa kwanza wa ligi hiyo uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Krmpotic alisema mchezo unaokuja ataanza kupanga mastaa wa kigeni akiwemo Tunombe Mukoko, Tuisila Kisinda na wengineo ili kukata kiu ya mashabiki walionekana kupiga kelele kwa kutowanzisha katika mechi iliyopita.
“Mchezo unaokuja utakuwa na mabadiliko ya wachezaji kwenye kikosi cha kwanza, kutakuwa na baadhi ya wachezaji ambao sikuwaanzisha kwenye mechi iliyopita na nafanya hivyo kutafuta ushindi wa kwanza,” alisema Krmpotic.
Aidha, alisema kilichosababisha kushindwa kuwapanga kwenye kikosi cha kwanza nyota hao wa kigeni katika mechi iliyopita ni kuchelewa kupata hati ya uhamisho wa kikazi wa Kisinda na Mukoko.
“Unajua kabla ya mchezo sikuwa na mpango wa kuwatumia wachezaji wa kigeni baada ya kukosekana vibali vyao vya kazi ambavyo vilipatikana mchana ndiyo maana asilimia kubwa niliwaanzisha wazawa,” alisema Krmpotic.
Alisema wachezaji wote wanaendelea kufanya mazoezi ya kutengeneza utimamu wa mwili kujipanga na mchezo unaokuja utakaofanyika tena Uwanja wa Mkapa.