Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Yanga amsifu Carlinhos

A51eeec5772fd544b5c0aec09f1daec4 Kocha Yanga amsifu Carlinhos

Tue, 15 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA wa Yanga, Zlatko Karmpotic, amesema Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ni mchezaji mzuri, lakini kwa sasa hajawa tayari kuonesha makali yake.

Carlinhos (pichani) ndiye aliyepiga kona iliyounganishwa kwa kichwa na Lamine Moro dakika ya 87 na kwenda moja kwa moja nyavuni na kuifanya Yanga kuzoa pointi tatu muhimu kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Karmpotic alisema licha ya mchezaji huyo kuonesha ubora wa kutumia vema mipira iliyokufa kwenye mechi hiyo, lakini hawajawa tayari kuingia kwenye mfumo, hivyo bado anamuandaa ili arejee kwenye makali yake.

“Carlinhos ni mchezaji mzuri bado namuaandaa sitaki kumuua, ila amekuwa akilazimika kutokea benchi, namuaandaa ili afiti kwenye kikosi kwani ana muda mrefu hajacheza mpira kwao Angola ambako alikaa kwa zaidi ya miezi mitano kwa sababu ya corona,” alisema Karmpotic.

Pia aliwagusia wachezaji wengine akiwemo Yacouba Sogne, akisema naye hajawa kwenye kiwango chake, kwani amekaa bila kucheza mpira kwa miezi minne, hivyo sio kazi rahisi kwa kocha kukitengeneza kikosi kwa mara moja anatakiwa kupewa muda wa kutosha kutengeneza muunganiko.

“Michael Sarpong kwenye mchezo wa leo (juzi) hajafunga, ni mchezaji mzuri, ameonesha mchango mkubwa kwa kutengeneza nafasi na kuwasumbua wapinzani wetu,” alisema.

Karmpotic alisema Tuisila Kisinda ni mchezaji mzuri, lakini kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City alishangazwa baada ya kuonesha kiwango cha chini.

Naye kocha wa Mbeya City, Amri Saidi, amewashukuru wachezaji wake kwa kucheza kwa nidhamu na kuzingatia mbinu alizowapa na kwamba kwa sasa wanaenda kujipanga kwa mchezo unaokuja dhidi ya Azam FC kutafuta ushindi na kurudisha morali.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kucheza kwa nidhamu na kuzingatia mbinu nilizowapa, tunakubali matokeo tunaenda kujipanga kwa mchezo unaokuja dhidi ya Azam FC kutafuta ushindi wa kurudisha morali na ari ya kikosi kupambana” alisema Saidi.

Ushindi huo umewafanya Yanga kufikisha pointi nne baada ya kutoka sare mechi ya ufunguzi kwa kufungana bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City hawana pointi kwani wamepoteza mechi zote baada ya kufungwa mabao 4-0 katika mechi ya ufunguzi dhidi ya KMC.

Chanzo: habarileo.co.tz