Siku kama ya leo 2008, aliyekuwa Kocha wa Yanga, Dusan Kondic aliwashukuru mashabiki wa klabu hiyo kwa sapoti huku akiwataka kila mmoja wao atoe sh 1000 kwa ajili ya kutunisha mfuko wa timu hiyo ulioyumba wakati huo.
Kondic raia wa Serbia aliliambia Mwanaspoti kwamba anajua Yanga ina mashabiki zaidi ya milioni 10 ila endapo watajitokeza milioni nne tu wakaamua kuwa wanachama na hata wakachangia dola moja ambayo ni sh 1,100 basi Jangwani watakuwa na uwezo wa kuingiza bilioni nne kwa mwaka bila ya kwenda uwanjani kusubiria mapato.
"Yanga ni tajiri kama wanachama wake wakiamua, wachezaji watakuwa wanapata kila wanachotaka, timu itapata kila mchezaji inayomtaka ila ni kama kila mmoja wao atajitokeza kujiandikisha uanachama na kutoa dola moja tu," alisema.
"Mimi sio kiongozi ila nimesomea mambo ya uongozi, nilifanya hivyo nikiwa Angola na nikashirikiana sana na viongozi, wanachama wajitokeze na kujiunga na timu ili fedha zao zitumike kwenye programu ya vijana ambayo itaifanya Yanga kuwa imara daima," alisema Kondic aliyewahi kufundisha soka Yugoslavia, Kuwait na Angola.
Ada ya uanachama ya Yanga ni sh 1000 kwa mwezi wa wamekuwa wakijiandikisha taratibu huku viongozi wao nao wakiendelea kuhamasisha wajitokeze.
Kondic alisema ufadhili wa Yusuf Manji ndio chachu ya kila kitu kwao hivyo unapaswa kupongezwa kwa hatua hiyo kubwa.
"Tunamshukuru Manji lakini tujiulize tutamtegemea hadi lini, halafu nafasi ya kujitegeme ipo labda kwa kuwa watu hawaelewi uongozi, uongozi uwaelimishe na wenyewe wajitekeze kwa wingi ili kuisapoti timu yao,"
"Wachezaji huongeza kujiamini wakijua wana uhakika wa kupata kila kitu, pia huongeza juhudi ya kujituma wakijua wanatimiziwa kila kitu hivyo huenda na deni uwanjani," alisema Kondic ambaye alizaliwa Aprili 1947.
Uongozi wa Yanga na watani zao Simba ambao hivi karibuni zilipata mkataba mnono kutoka bia ya Kilimanjaro wamekuwa wakiomba wanachama kujitokeza kwa wingi ili kuziwezesha timu hizo kuwa na uwezo wa kujitegemea kupitia fedha zao na sio za wafadhili tu.