Akiwa kwao America lakini kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amepitisha usajili wa winga mmoja anayejua kutupia asisti za maana akisema anataka amkute mjini kabla ya hajafika.
Kocha Gamondi amepitisha usajili wa winga Maxi Nzengeli, akisema baada ya kukatwa kwa Mkongomani Tuisila Kisinda amepewa faili la winga huyo kisha kubariki fasta akisema anataka mashine hiyo itue haraka kabla hawajaanza kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Tayari mabosi wa Yanga wameshaanza mazungumzo na klabu ya Union Maniema ambao ni marafiki zao wakiwa katika mudi nzuri ya kuuziana wachezaji ili kukamilisha dili hilo.
Hii ni mara ya pili kwa Yanga kumpigia hesabu Maxi ambaye ni nahodha wa kikosi cha Maniema kinachomilikiwa na bosi mmoja mkubwa wa jeshi la DR Congo.
Maxi mwenyewe ameshaliamsha kwa mabosi wa klabu hiyo akiwataka kumalizana na Yanga haraka ili asikwame kama mbavyo alikwama msimu uliopita kataka dirisha kubwa la usajili kama hili.
Staa huyo mtaalam wa pasi ameliambia Mwanaspoti kuwa ni habari njema kwake kwa Yanga kurudi tena kuhitaji huduma yake na kwamba anachosubiri sasa ni kumalizika kwa mazungumzo ya pande hizo mbili.
"Viongozi wangu wa Maniema wamenifuata kunijulisha kwamba kama niko tayari kuhamia Yanga nimewaambia, hakuna shida kitu muhimu wao wamalizane nao haraka niondoke,"alisema Maxi.
"Yanga ni klabu kubwa wako wakubwa zangu wanacheza huko tunaona jinsi mafanikio yao yanavyozidi kuwa makubwa, bahati mbaya huku kwetu ligi imekuwa haieleweki itakuwa vyema kama nitakwenda Yanga ili nikacheze mashindano makubwa."
Yanga inataka kukamilisha dili hilo haraka kumpata Maxi kuja kuimarisha eneo la winga wao wa kulia ambalo sasa limebaki na watu wawili pekee Jesus Moloko na Denis Nkane baada ya kuwaondoa Kisinda na mzawa Dickson Ambundo.