Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps wala hana wasiwasi na kitendo cha kikosi chake kushinda kuwasha moto kwenye fainali ya Euro 2024 hasa katika mechi zao mbili za kwanza walizocheza kwenye hatua ya makundi.
Les Bleus imekuwa ikicheza kama timu isiyokuwa na nafasi kubwa ya kunyakua taji hilo, ambapo hadi sasa imefunga bao moja tu, tena bao lenyewe ni la wapinzani kujifunga.
Katika mechi ya kwanza, Ufaransa ilikipiga na Austria, ndipo ilipopata ushindi kupitia bao la kujifunga, huku wakipata gundu la kumpoteza supastaa wao, Kylian Mbappe, ambaye alivunjika pua.
Kwenye mchezo wao wa pili, uliofanyika Leipzig Ijumaa iliyopita ilipokwaruzana na Uholanzi, timu hiyo ilitengeneza nafasi nyingi, lakini ilishindwa kuzitumia kutumbukiza mpira nyavuni, kupitia kwa mastaa wake makini kama Antoine Griezmann.
Nafasi nyingine ya kufunga alipata kiungo Adrien Rabiot, lakini alishindwa kutupia nyavuni na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 0-0.
Lakini, Deschamps, ambaye kikosi chake kitacheza na Poland kwenye mechi ya mwisho ya makundi, alisema: "Tutakwenda kuboresha mambo kwenye safu yetu ya ushambuliaji. Kuna vitu vingi vinavyotupa imani. Ni kitu cha wazi, ukitaka kushinda mechi, unahitaji kufunga mabao.
"Tunaamini tutaboresha ubora wetu kwenye mechi ijayo. Ningepata wasiwasi sana kama tungekuwa hatutengenezi nafasi."
Kushindwa kupata ushindi kwenye mechi ya Uholanzi, kumefanya Ufaransa kufikisha mechi saba bila ya kushinda, kila ambapo supastaa Mbappe hakucheza. Staa huyo alikosa mchezo huo kutokana na kuuguza jeraha la kuvunjika pua.
Na sasa, straika Olivier Giroud ambaye amekuwa kwenye benchi katika mechi zilizopita, anatazamiwa kupata nafasi katika mechi hiyo ya kuwakabili Poland itakayofanyika leo Jumanne huko Dortmund.