Kocha msaidizi wa timu ya taifa, Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco', amefichua jambo akisema amezungumza na kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' aliyeikaushia kambi ya Yanga akimtaka arejee klabuni hapo, ili kujihakikishia namba Stars kwani watamtathimini kabla ya kuitwa tena baadae.
Fei yupo nje ya Yanga tangu alipotangaza kuvunja mkataba na klabu hiyo na kuilipa Sh 112 Milioni zikiwamo za mishahara ya miezi mitatu, lakini klabu hiyo ikamgomea na kukimbilia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji inayomtambua ni mali ya timu hiyo.
Hata hivyo, licha ya kutokuwa na timu tangu Desemba makocha wa Stars walimuita na kumjumuisha kiungo huyo kwenye kikosi kilichocheza mechi mbili za kuwania tiketi za Afcon dhidi ya Uganda na ukizuka mjadala juu ya kiwango chake, lakini Morocco amevunja ukimya na kuzungumza mipango ya benchi la timu hiyo kwa mchezaji huyo kwa mechi zijazo baada ya kuzungumza naye.
Akizungumza Morocco alisema kama makocha wataangalia namna ya kumtumia Fei kwa mechi zilizozalia kundini katika mchujo huo wa kwenda Ivory Coast na kuweka bayana kwamba alizungumza naye ili kumpa ushauri wa kipi cha kufanywa kwa sasa kulinda kiwango chake.
Morocco alisema kwa vile kuna miezi miwili mbele kabla ya Stars kucheza mechi za mwisho za Kundi F ikiwamo ya nyumbani dhidi ya Niger na ile ya kufungia dimba na vinara na timu iliyofuzu mapema kwenda Afcon, Algeria wataangalia kama itawezekana kumtumia kiungo huyo au la. "Tuna mechi tena mwezi wa sita hapa kuna miezi miwili chochote kinaweza kutokea tutafanya tathmini na kama tutaridhika tutaona,"alisema kocha huyo kutoka visiwani Zanzibar.
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Coastal Union, Morocco na nyingine kwenye Ligi Kuu Bara alisema kama kocha alizungumza na Fei na kumpa kitu cha kufanya ikiwamo kukilinda kiwango chake, japo wenye mamlaka ndio wenye maamuzi ya mwisho.
"Kama kocha nimejaribu kuzungumza naye, lakini unajua haya mambo yanaendeshwa na mamlaka na watu wanaomsimamia Fei, hivyo ebu acha kwanza tuone kinachofuata, ila kuna mambo nimemshauri," alisema Morocco.
Fei aliingiza kwenye mzozo na klabu hiyo Desemba 2 4alipandika barua ya kuaga kupitia akaunti za mtandao ya kijamii, kisha kuiingizia Yanga Sh 112 Milioni za kuvunja mkataba kabla ya mabosi wa Yanga kumburuza TFF iliyomtambua ni mchezaji halali wa klabu hiyo na kumtaka ajiunge nao.
Upande wa Fei haukukubaliana na maamuzi hayo na kuomba marejeo ya kesi hiyo ambayo hata iliposikilizwa tena ilisisitiza alivunja mkataba kienyeji na bado ni mchezaji halali na mwishowe uongozi ukasema upo tayari kukaa naye na kuzungumzia masilahi anayoyataka ili mambo yaishe.
kiungo huyo aliomba kuzungumza na uongozi wa Yanga ili mambo yaishe, hata hivyo lilikwama.