Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Stars awekwa kiporo na TFF

Adel Amrouche Stars Kocha Stars awekwa kiporo na TFF

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha mkuu wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Adel Amrouche akihojiwa na mwandishi wa habari za michezo nchini Algeria Mohamed Chikhi kupitia Television ya SAT TV ameweka wazi kuwa timu ya Taifa ya Morocco imekuwa ikijipangia marefa wanaowataka kuchezesha mechi zao.

Adel ameendelea zaidi kwa kusema hata katika mchezo wa kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za kombe la Dunia uliofanyika Dar Es Salaam Morocco ilikuja na marefa wake ambao muda wote walikuwa upande wa Morocco kwenye maamuzi ndani ya uwanja.

Kikawaida shirikisho la soka Barani Afrika CAF lenyewe ndilo lenye mamlaka ya kuteua waamuzi wa mchezo husika ambao upo kwenye kalenda ya shirikisho hilo.

“Morocco inaamua kila kitu katika soka la Afrika, pia wanachagua waamuzi wao, Tunabaki kuwa watazamaji kwasababu wanaamua kila kitu, Sitashangaa yakijirudia haya katika mchezo ujao wa AFCON dhidi yao”, Alisema Adel Amrouche, Kocha mkuu wa kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania [Taifa Stars].

Baada ya kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania Adel Amrouche kutoa kauli zile, Rais wa shirikisho la soka nchini Tanzania Wallace Karia ametoka hadharani na kusema kile alichokisema kocha shirikisho halijui ni maoni yake Binafsi.

Hata hivyo Rais Karia ameweka wazi kuwa kwasasa hawatamuuliza chochote kwasababu yupo kambini na wakifanya hivyo wamaweza kuiharibu kambi ya timu ya Taifa.

Karia amesema pindi michuano itakapomalizika basi kama shirikisho watachukua hatua na watazungumza nae ili asiwe anatoa kauli zitakazoligombanisha shirikisho la soka Tanzania na CAF.

“Sisi kama TFF hatukubaliani na hizo kauli, hizo kauli kazitoa kocha mwenyewe binafsi, sisi tupo ndani ya CAF, tunajua CAF wanafanya kwa utaratibu sio shinikizo la nchi yoyote”.

“Shirikisho la Morocco na Tanzania ni marafiki, hili litabaki ni la kwake mwenyewe, tuko mbali na kauli zake na hatuzikubali”.

“Tutajua tutafanya nini, tuko kwenye mashindano, kuchukua hatua ambazo tutaona zinastahili kuchukuliwa”.

“Pia tutaongea nae ili ajizuie kwenye kauli zake asije akatuletea matatizo sisi na wenzetu”, Alisema Rais wa TFF, Wallace Karia.

Taifa Stars ina mchezo muhimu kesho dhidi ya timu ya Taifa ya Morocco kwenye fainali za mataifa ya Afrika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live