Simba inaenda nchini Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa ambapo wao wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika huku wakiwa na kocha wao mpya, Zoran Mako akienda moja kwa moja nchini humo.
Simba imeingia mkataba wa na kocha huyo raia wa Serbia ambaye amepewa malengo ya kurejesha heshima ya Simba ikiwemo mataji matatu ya ndani waliyoyapoteza pamoja na kufanya vizuri zaidi michuano ya kimataifa.
Simba imepoteza taji la Ngao ya Jamii, Ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambayo yote yametwaliwa na watani zao, Yanga.
Wakati wanafanya maandalizi ya kambi hiyo lakini Mako hatakuja nchini na wasaidizi wake huku habari zikieleza kwamba viongozi wapo kwenye mchakato wa kusaka kocha wa makipa na mtaalamu wa viungo.
Simba inatarajia kuondoka nchini katikati ya Julai huku wachezaji wote wanatakiwa kuwasikili Dar es Salaam Julai 13 mwaka huu tayari kwa maandalizi ya mwisho ya safari hiyo.
Hivi karibuni, aliyekuwa kocha wa makipa wa timu hiyo Tyron Damons aliachana na timu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika na kupata ofa nono timu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Mbali na huyo pia iliachana na kocha mkuu Pablo Franco na kocha wa viungoo Daniel Castro ambaye anatafutiwa mbadala wake.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano cha Simba, Ahmed Ally alithibitisha juu ya hilo kuwa; “Kocha atakutana na timu huko huko kambini ambako tunaenda kwa ajili ya ‘pre season’ maana kwasasa hata akija hapa hakuna cha kufanya kwani wachezaji wamepewa mapumziko, hivyo kwa asilimia kubwa ataenda kambini moja kwa moja.”
Alisema wachezaji watakutana jijini Dar es Salaam huku akisisitiza usajili wao unaendelea na utakapokamilika kila kitu kitawekwa wazi. Hadi sasa, Simba wamemtangaza rasmi mchezaji mmoja Moses Phiri huku wengine wakielezwa kumalizana nao ambao ni Augustino Okra, Habibu Kyombo, Ceasar Lobi Manzoki, Nassoro Kapama pamoja na Victor Akphan.