Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara, Simba SC, Seleman Matola, amesema magumu ambayo wanayapitia kwa sasa yana muda, kwa kuwa wanapambana kurudi kwenye ubora uliozoeleka.
Simba SC imeshacheza michezo mitano ya Ligi Kuu msimu huu 2021/22, imeshinda michezo mitatu na kupata sare mbili huku kinara wa ufungaji kweye klabu hiyo hadi sasa ni Meddie Kagere mwenye mabao mawili.
Matola amesema wanatambua kikosi chao kinapitia kipindi kigumu ila kuna mwisho kwa kuwa kinachowasumbua kipo wazi, na wapo mbioni kukitafutia ufumbuzi wa kudumu.
“Ipo wazi kwamba kwa sasa tunapitia kwenye wakati mgumu lakini haya mapito yana mwisho hayatadumu siku zote. Nilikuwa mchezaji wa Simba na niliwahi kukutana na mambo kama haya.”
“Licha ya hivyo hata msimu uliopita pia tulipitia kwenye kipindi kama hichi lakini mwisho wa siku tukarejea kwenye ubora na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, mashabiki wasikate tamaa waendelee kuwa nasi kama ambavyo kwa sasa wanafanya,” amesema Matola.
Ushindi huo umeiwezesha Simba kufikisha alama 11 na kukwea hadi nafasi ya pili kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Young Africans wakiwa kileleni kwa kufikisha alama 15.