Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Ruvu Shooting acharuka "Wachezaji hawajitumi"

Ruvu Shootinggggg Kocha Ruvu Shooting acharuka

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya Ruvu Shooting kucheza mechi sita mfululizo bila kupata ushindi kocha wa timu hiyo Khalid Adam amedai tatizo ni wachezaji wake ambao hawajitumi.

Licha ya kuwa na nyota kadhaa wenye majina na uzoefu kama Miraji Athuman 'Sheva', Jaffary Mohamed, Mohamed Ibrahim, Ludovick Charles, Hassan Isihaka na wengine wengi lakini imekuwa uchochoro wa timu zingine za Championship kujichukulia pointi kiulaini.

Ruvu ilianza kupoteza dhidi ya FGA Talents (2-1), Polisi Tanzania (1-0), Ken Gold (0-3), Mbeya City (0-1), Mbeya Kwanza (1-0), kabla ya kupokea kichapo kizito dhidi ya Mbuni FC cha mabao 5-0 mchezo uliopita.

Akizungumza nasi, Adam amesema tatizo siyo lake kwasasa na wala hapaswi kulaumiwa kutokana na matokeo mabaya ambayo timu hiyo imepata hadi sasa bali wachezaji aliyonao ndio hawajitumi na hawana moyo wa kupambana.

Amesema walifanya maandalizi japo kwa kuchelewa na mambo yakawa yanaenda vizuri hadi kucheza ugenini dhidi ya Mbeya Kwanza vijana wake walikuwa wanaonyesha kweli kuna kitu lakini bado anashangaa kwenye mechi mambo yanakuwa ni yale yale.

“Ndio tulichelewa kufanya maandalizi lakini timu ilishafika kwenye 'pick' siwezi kulaumu tena habari ya maandalizi sasa hizi nalaumu wachezaji wangu ambao hawajitumi,” amesema Adam.

Aliongeza kuwa amekuwa akifanyia kazi jambo moja kila siku lakini bado yanajirudia yaleyale hivyo anafikiri hawamsaidii kwa sababu wanacheza bila moyo wa upambanaji.

“Nimeikuta hii timu sikutaka kukataa kwa sababu watu ambao waliniita nawaheshimu, napambana kwa sababu kazi yangu ni kufundisha siyo lazima nifundishe sasa hivi nipate matokeo Ligi bado ndefu kupata matokeo mazuri inawezekana na tukapanda Ligi Kuu moja kwa moja au kwa play-off”,” alisema Adam.

Akizungumzia mustakabali wake ndani ya kikosi hicho amesema bado yupo yupo sana kama kocha nafasi yake bado ipo ataendelea kuwa nao wala hajachoka na kuweka wazi kuwa kama angekuwa kocha mwingine tayari angeshakimbia siku nyingi sana.

Amesema malengo ni kupanda Ligi Kuu hivyo atatumia dirisha dogo la usajili kuweza kuongeza nguvu mwenyewe kwa sababu hii timu ameikuta tu na tayari ashajua wapi kuna mapungufu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live