Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha: Pacome na Chama? Naenda na huyu!

Pacome Chama Pc Kocha: Pacome na Chama? Naenda na huyu!

Sat, 2 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kuibuka kwa maswali juu ya nani ni bora zaidi kati ya Pacome Zouzoua wa Yanga na Clatous Chama wa Simba, Kocha wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Juliet Chevalier amekata mzizi wa fitina kwa kutoa jibu alipozungumza na Mwanaspoti.

Kocha huyo, aliyemnoa Pacome msimu uliopita katika kikosi cha Asec aliyemaliza msimu kwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora akifunga mabao saba na kuasiti nne, kabla ya kutua Yanga msimu huu, amesema kwa bahati nzuri wachezaji hao wawili anawajua, kwani Chama ameshakutana msimu huu kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Asec na Simba zilipangwa kundi moja la B katika makundi ya michuano hiyo ya CAF na katika mechi mbili baina yao ziliisha bila kutoa mshindi, mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam uliisha kwa sare ya 1-1 na ule wa wiki iliyopita mjini Abidjan, Ivory Coast zilitoka suluhu, Chama akiwamo kikosi kwenye mechi zote mbili.

Hivyo, kocha huyo anafahamu vizuri uwezo wa wachezaji hao wanamudu nafasi ya kiungo mshambuliaji na kusema kama ni kutaka kuamua nani mkali kati yao, basi yeye angempa kura, Pacome kwani anajua sana, japo amekiri Mzambia wa Simba naye sio wa kubeza na kwa sasa anaangushwa na umri alionao.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema hakuna kocha atakayepewa Pacome akamkataa, kwani ni mchezaji bora sana na hata akitua Simba hawezi kukosa namba.

Alikiri anamjua Chama amekutana naye karibu mara tatu, lakini amefanya kazi na Pacome na sasa haoni kama ni sahihi kwa mchezaji huyo wa zamani wa Asec kulinganishwa kwa sasa kwa uwezo na staa huyo wa Msimbazi.

"Chama anachomzidi ni kukaa muda mrefu ndani ya Simba na uzoefu katika Ligi ya Tanzania, pia amecheza muda mrefu kidogo kuliko Pacome. Ila kwa ubora hawezi kumpata kwani kiungo wa Yanga ana vitu vingi ambavyo anaweza kukupa uwanjani ikiwemo kasi, nguvu, ingawa wote wanakuja kulingana katika matumizi ya ufundi na akili ya kufunga," alisema Chavalier na kuongeza;

"Pacome ni suala la muda, atakuja kuwa kiungo hatari zaidi ndani ya soka la Tanzania na Afrika kwa jumla kutokana na ubora alionao."

Rekodi zinaonyesha Chama aliyeanza safari ya soka msimu wa 2013-2014 akiwa wamecheza muda mrefu zaidi ya Pacome aliyeanza msimu wa 2016-2017, hivyo kutofautiana hata idadi ya timu walizozitumikia.

Chama hadi sasa ameshachezea timu nane wakati Pacome kazichezea saba, pia wanatofautiana umri walionao, Triple C akiwa na miaka 32, ikiwa ni sita zaidi ya aliyonayo kiungo mshambuliaji huyo wa Yanga mwenye 26.

Katika msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Pacome amefunga mabao matatu na kuasisti moja akishika nafasi ya pili nyuma ya raia mwenzake wa Ivory Coast aliyekuwa Asec, Sankara Karamoko aliyeuzwa Ulaya kwa sasa, huku Chama akiwa hana bao, japo leo usiku atakuwa na nafasi wakati Simba ikimalizana na Jwaneng Galaxy.

Simba na Jwaneng kutoka Botswana zinapepetana kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni mechi ya mwisho ya Kundi B huku timu hizo pamoja na Wydad inayocheza na vinara Asec zikiwa na nafasi ya kutinga robo fainali kuwafuata Waivory Coast iliyopenya mapema ikiwa na pointi 11.

Chanzo: Mwanaspoti