Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Nassor aanika mkasa dawa kulevya Mauritius

100786 Pic+dawa Kocha Nassor aanika mkasa dawa kulevya Mauritius

Mon, 30 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ilikuwa ni taarifa ya mshituko kila Mtanzania hakutarajia kilichotokea, kocha wa timu ya Taifa ya ngumi za ridhaa na mabondia wake kukamatwa nchini Mauritius.

Ni miaka 11 na miezi kadhaa sasa imepita, lakini Nassor Michael aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa anasema hawezi kusahau.

Akiwa ameambatana na mabondia wawili, Emmilian Patrick na Petro Mtagwa nchini Mauritius kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya Olimpiki ya 2008 iliyofanyika Beijing, China, Nassor na msafara wote wa Tanzania ulikamatwa.

Watanzania hao walituhumiwa kula njama na kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine nchini humo.

Wakati ule Emmilian alikuwa amefuzu kushiriki Olimpiki, Mtagwa aliambatana naye kambini kama msaidizi wa mazoezi ya kupigana ana kwa ana (sparing patner), Nassor na watu wengine watatu.

“Wale watu wengine niliambiwa ni wadau wa ngumi na ndiyo walikuwa wadhamini wetu hata hivyo tulikutana nao uwanja wa ndege,” anasimulia Nassor alipozungumza na gazeti hili.

Pia Soma

Advertisement
Anasema baada ya kuondoka Dar es Salaam walipitia Kenya na kwenda Mauritius.

“Tulikuwa salama tulifika hadi hotelini tukiwa vizuri ghafla nikiwa chumbani kwangu ndipo nikawekwa chini ya ulinzi na askari wa Mauritius.

Anasema wakati huo wale wadhamini wao na mabondia pia walikuwa wamekamatwa.

“Sikujua nini kinaendelea hadi nilipofikishwa kituoni tukaambiwa tunatuhumiwa kusafirisha dawa za kulevya,” anasema.

Habari ya mjini ilikuwa ni tukio hilo, hapa nchini aliyekuwa rais wa Chama cha Ngumi wakati ule, Alhaji Shabani Mintanga alikamatwa na kuwekwa mahabusu wakati upelelezi ukiendelea. Habari zaidi UK 16

Maisha mapya jela ugenini

Nassor anasema kesi yao haikuwa na dhamana hivyo walipelekwa mahabusu nchini humo na kuanza maisha mapya.

“Nilikuwa mtuhumiwa namba moja kila mshitakiwa tuliyekuwa naye anasema mimi ndiye niliyewapeleka Mauritius,”.

Anasema wakati huo hakujua lolote na hakujua namna ya kujitetea, lakini kama kocha ambaye aliambatana na wachezaji alisimama imara.

“Kilikuwa kipindi kigumu kwangu, lakini Mungu alinivusha niligeuza jela kuwa kanisa nilijutia kwanini nilimuacha Mungu na kuingia kwenye mchezo wa ngumi sikuwa na namna,” anasema.

Jela Mauritius kama hoteli

Nassor alikuwa Mtanzania wa pili kuachiwa huru baada ya Emmilian Patrick. Alikaa jela tangu mwaka 2008 hadi 2011 alipoachiwa.

Licha ya kukosa uhuru anasema akiwa jela alipata kila kitu alichokuwa akihitaji ikiwamo kulala chumba cha peke yake ambacho ni ‘self’ na chakula bora.

“Nilipata huduma karibu zote muhimu ilikuwa kama naishi hotelini kila kitu kilikuwepo nilikuwa nikitaka chumba cha peke yangu napewa cha wawili, watatu hadi wanne.

“Achana na kulala, chakula cha jela ya kule ni zaidi ya nilichokuwa nakula nyumbani,” anasema Nassor.

Anasema siku ya kwanza kuingia jela walipewa kila mmoja shuka mbili, blanketi mbili na mto.

“Ratiba ya chakula asubuhi katika chai tulipewa yai moja moja, mimi kwa ucheshi wangu nilikuwa napewa mayai mawili kila siku.

Anasema ratiba ya mchana ilikuwa lazima kuwe na samaki na kuku au nyama ya ng’ombe na vivyo hivyo usiku.

“Tulikosa tu mboga za majani kwani kule mboga mboga ni bei juu kama ambavyo unanunua Tanzania maini, lakini kuku, samaki, nyama ya ng’ombe au mbuzi ilikuwa ni kitu cha kawaida,” anasema.

Anasema kwa wavuta sigara walikuwa wakiletewa gerezani na ilikuwa ni ratiba ya kila siku.

“Mimi kwa kuwa nilikuwa sivuti sigara zangu nilikuwa nikibadilishana na wanaovuta kwa mapaja ya kuku wakati wa chakula sahani yangu ilikuwa inasheheni,” anasema bondia huyo nyota wa zamani wa ngumi za uzito wa juu.

Anasema alikuwa akila vizuri tofauti na ilivyokuwa nyumbani alinenepa, ingawa kilichomsumbua ni kukosa uhuru.

“Ile nchi jela zao ziko tofauti kuna wafungwa wa mataifa mengine tuliwakuta kule walikuwa wanagoma kutoka gerezani.

“Kuna mmoja aliwahi kujipaka kinyesi ili asipelekwe mahakamani ambako alikuwa akienda kuachiwa huru sababu ya maisha ya jela za kule hadi biashara zinafanyika gerezani,” anadokeza.

Siku anaachiwa mambo yalikuwa hivi

Nassor anasema licha ya gerezani kuwa ya kawaida, lakini alisumbuliwa na fikra ya familia yake nchini Tanzania kibarua chake na uhuru.

“Niliomba Mungu nitoke kweli alinijibu kwani siku chache kabla ya kuachiwa niliota ndoto niko nyumbani Tanzania.

Anasema baada ya Emmilian kuachiwa huru alipowaaga alimwambia naye atakuwa nyuma yake kurudi Tanzania siku si nyingi.

“Nakumbuka siku moja kabla ya kupelekwa mahakamani, askari wa gereza aliniita akaniambia nenda kwenye gala usogeze vitu vyako.

“Utaratibu wa kule kuna eneo ambalo ukiwa gerezani mnatunzia vitu vyenu, hivyo nilipoambiwa hivyo nikajua siku yangu ya kutoka jela imewadia.

Anasema siku iliyofuatia akiwa mahakamani hakimu alisema hana hatia hivyo yuko huru kwani hakuna ushahidi wa kumtia hatiani.

“Nilipiga magoti kumshukuru Mungu pale mahakamani, sikuamini,” anasema. Anasema kipindi chote cha kesi yao hakuwa akijibu chochote mahakamani kwani hakuna alilojua na ndivyo ilikuwa kwa Emmilian ambaye aliachiwa wa kwanza.

“Nilirudi kuwaaga wenzangu Petro alinisindikiza hadi mlangoni wakati natoka jela nilimtia moyo nikamwambia naye atatoka tu, hawakuamini kuona mimi mtuhumiwa namba moja naachiwa huru, kwani wote walisema mimi ndiye niliwapeleka,” anasema.

Petro na watu wengine watatu walihukumiwa na mpaka sasa bado wanaendelea na kifungo nchini humo ambacho kinaelekea ukingoni.

Safari ya kurudi Tanzania ilivyokuwa

Nassor anasema hatoacha kumshukuru na kumtukuza Mungu kwani ndiye kila kitu kwani hakutarajia kukanyaga ardhi ya Tanzania na kuungana na familia yake.

“Nilifanyiwa taratibu zote nikarejeshwa nchini nilikaa kwa muda kidogo kabla ya kurudishwa kazini Jeshini,” anasema.

Amtaja Muhammad Ally

Nassor anaeleza namna alivyoanza ngumi mwaka 1970 wakati huo akiwa mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

“Nilikuwa nikivutiwa na kiwango cha Muhammad Ally, wakati ule ili kupata fursa ya kumuona lazima uende sinema.

“Nilipomuona kwa mara ya kwanza, kipindi hicho nilikuwa nacheza soka nikajikuta navutiwa na ngumi nikaanza kumfuatisha namna alivyokuwa akirusha ngumi na kukwepa. “Nilikuwa nafanya hivyo huku nikijitazama kwenye kioo nyumbani baadaye nikaanza kujifunza mazoezi rasmi nikielekezwa na bondia Mashauri Changarawe (mdogo wa Michael Changarawe).

Enzi zake Nassor hakuwahi kupigwa nchini

“Nilianza kujifunza kupiga begi, padi, kipindi hicho sikuwa na aidia ya ngumi,” anasimulia.

Anasema pambano lake la kwanza alicheza mwaka 1972 na bondia aliyemtaja kwa jina moja la Ally ambalo lilipigwa Temeke ambaye alimpiga hadi akakimbia ulingoni.

Titus Simba ampa umaarufu

Nassor ambaye alikuwa staa wa ngumi nchini tangu mwaka 1973 hadi anastaafu mwaka 1993 anasema, pambano na bondia mwenye historia ya pekee nchini, Titus Simba ndilo lilimpa heshima.

“Wakati ule Simba alikuwa na historia ya kuwa bondia wa kwanza Mtanzania kuiletea nchi medali ya kimataifa (alishinda medali ya fedha ya Jumuiya ya Madola mwaka 1970).

“Alikuwa akipigania uzani wangu, lakini tulikwepana kupigana, ikatokea tumeandaliwa pambano Dodoma lilikuwa gumzo nilimpiga Simba KO raundi ya pili,” anasema.

Alimpiga Koba Kimanga

Licha ya Koba Kimanga kukiri kumuogopa Nassor ambaye wakati huo amepangwa kucheza naye, Nassor alikuwa staa, bondia huyo anasimulia namna alivyozichapa na Koba bila kufanya mazoezi.

“Nilikuwa nimetoka Ulaya kwenye pambano nimeenda likizo nyumbani Musoma, kocha wa timu ya Taifa raia wa Burgaria akanipa taarifa kwamba napaswa kurudi ili nije nipigane na Koba Kimanga.

“Nilimwambia sina mazoezi akasema utashinda nikakubali nikarudi sikuwa na mazoezi ila nilipanga kutumia mbinu ya kumpeleka chini raundi ya kwanza mara tatu ili refarii amalize pambano.

Anasema mbinu hiyo kweli ilifanikiwa sekunde ya 10 Koba alikwenda chini kwa konde akanyanyuka akasema anaendelea akampa ngumi nyingine ya kulia ikampeleka chini, Koba akanyanyuka akasema anaendelea hadi raundi ya kwanza inakwisha Koba alipelekwa chini mara tatu.

Katika simulizi ya Koba anasema, msaidizi wake ulingoni (second) alirusha taulo ulingoni kwa lengo la kumuokoa, lakini yeye akalirusha nje kwa mguu na kusema anaendelea.

“Wakati ule Nassor alikuwa staa, nilijitutumua sikutaka kupigwa KO nilicheza na kumaliza raundi zote na Nassor alishinda kwa pointi,” aliwahi kusimulia Koba katika moja ya makala na Spoti Mikiki.

Nassor anasema katika maisha yake akiwa bondia wa timu ya Taifa kwa miaka 20 hakuwahi kupigwa na mabondia wa Tanzania ingawa nje alipigwa.

Kocha

Baada ya kustaafu Nassor alisomea ukocha na kupewa mikoba ya kuinoa timu ya ngumi ya Taifa tangu mwaka 1996 hadi 2008. Katika kipindi chake cha ukocha aliiwezesha Tanzania kutwaa medali ya dhahabu ya Jumuiya ya Madola iliyoletwa na Michael Yombayomba mwaka 2006.

“Nilikuwa nikitumia mbinu zangu kuwanoa mabondia wa timu ya Taifa, ndiyo sababu wengi wao walifanya vizuri kabla ya ngumi kuanza kupotea kimataifa tangu 2008 tulipopata matatizo,” anasema.

Historia yake kimataifa

Nassor aliyezaliwa Julai 13, 1956, ameiwakilisha nchi kwenye Olimpiki ya mwaka 1980 na 1984, michezo ya Jumuiya ya Madola ya 1982 na michezo kadhaa ya Afrika katika uzani wa light heavy.

Katika Olimpiki ya 1980, mabondia tisa waliiwakilisha nchi, wengine ni William Isangula (heavy), Leonidas Njuwa (light middle), Lucas Msomba (welter), Omari Golaya (light), Isack Mabushi (bantam), Feraldi Issack (bantam) na Emmanuel Mlundwa (fly) ingawa wote hawakufanya vizuri.

Nassor amewahi kuwa bingwa wa dunia wa majeshi, mchezaji bora wa Afrika na bingwa wa nchi za ujamaa na mshindi wa pili wa Afrika katika uzani wa light heavy.

Chanzo: mwananchi.co.tz