Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasredine Mohamed Nabi amefichua kinachomsibu Nahodha na Beki wa kikosi chake Bakari Nondo Mwamnyeto.
Tangu msimu huu 2022/23 ulipoanza mwezi Agosti, Mwamnyeto amekosa muendelezo wa kucheza kwa kiwango cha ushindani, kama ilivyokua msimu uliopita, hali iliyopelekea kukosa baadhi ya michezo ama akitumika kama mchezaji wa akiba.
Nafasi ya Beki wa kati kwa sasa imekua ikitumikiwa na Beki kutoka DR Congo Yennick bangala akisaidiana na Mtanzania Dickson Job.
Kocha Nabi amesema Beki huyo aliyesajiliwa klabuni hapo akitokea Coastal Union misimu miwili iliyopita anakabiliwa na changamoto ya Msongo wa Mawazo, hali inayopekea kukosa kujiamini anapokua Uwanjani.
Amesema kinachofanywa hivi sasa ni kuhakikisha anarejea katika kiwango chake ili aweze kuisaidia timu katika kipindi hiki, ambacho wanapambana ili kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara na kufika hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
“Sikupaswa kulieleza lakini watu wafahamu mchezaji anaweza kukutana na mambo magumu hata nje ya uwanja, alikuwa akiuguliwa na mzazi wake, tumekuwa tukijitahidi sana kuwa naye karibu na hata kumsaidia na tunaona anaimarika taratibu.” amesema Kocha huyo kutoka Tunisia
Young Africans leo Jumatatu (Oktoba 03) itashuka Dimbani (Uwanja wa Benjamin Mkapa) jijini Dar es salaam kucheza dhidi ya Ruvu Shootingi majira ya saa moja usiku.