Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Nabi achimba mkwara Young Africans

Nasreddine Nabi Kazi Nabi na Kaze

Fri, 16 Sep 2022 Chanzo: dar24.com

Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Nesreddine Nabi, amewahimiza wachezaji wake kuwa tayari kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC kesho Jumamosi (Septemba 17).

Young Africans itakua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiwa na mtaji mkubwa wa mabao 4-0 waliouvuna katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanjani hapo mwishoni mwa juma lililopita.

Nabi amesema amewataka wachezaji wake wajitathmini ubora wao kwa sababu ya ushindani uliopo mbele yao katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano hayo ya kimataifa wanayoshiriki.

Nabi amesema mchezo wa kesho Jumamosi hautakuwa rahisi hivyo anawakumbusha wachezaji kufanyia kazi maelekezo yote anayowapa wanapokuwa katika mazoezi kwa sababu mchezo huo hautakuwa mwepesi kutokana na wapinzani wao kuzoea mazingira.

Kocha huyo amesema licha ya ushindi mnono wa mabao 4-0 walioupata katika mechi ya kwanza, hafurahishi na namna ambavyo wachezaji wake wanavyopoteza nafasi za kufunga zinazotengenezwa.

Amesema ushindi walioupata katika mchezo wa kwanza sio kigezo cha wao kushinda mchezo wa kesho, wanatakiwa kupambana zaidi na kuongeza umakini ili kutumia vyema nafasi watakazozipata.

“Sio kwa sababu tulishinda katika mchezo wa kwanza, huu wa marudiano utakuwa mwepesi, tunatakiwa kuongeza umakini ikiwamo kuwajenga kisaikolojia wachezaji na kuamini utakuwa ni mchezo mgumu kuzidi ule wa awali,” amesema Nabi

Ameongeza wachezaji wanatakiwa kuingia uwanjani kwa makini kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huu ambao ni muhimu ili waweze kufikia malengo yao.

“Haya ni mashindano ambayo unatakiwa kutumia nafasi ambazo unatengeneza, nafahamu huwezi kufunga katika kila nafasi, nafahamu tupo katika timu ambayo ina presha ya kupata matokeo, lakini mchezaji lazima uwe na utulivu unapofika lango la wapinzani, ukivaa jezi ya Young Africans lazima ucheze kwa akili na kujitathmini,” ameongeza kocha huyo kutoka nchini Tunisia.

Mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Young Africans dhidi ya Zalan FC atakutana Mshindi wa mchezo kati ya St. George FC ya Ethiopia au Al Hilal ya Sudan.

Chanzo: dar24.com