Dozi ya mazoezi mara mbili kwa siku, inaaminiwa na Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, huenda ikawa suluhisho la kurejesha mpango wa kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuibanjua Al Hilal nyumbani kwao Sudan.
Young Africans ina deni la kwenda kushinda ugenini mwishoni mwa juma hili, baada ya kualazimishwa matokeo ya sare ya 1-1 ilipocheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam mwishoni mwa juma lililopita (Oktoba 08).
Kabla ya kucheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza Jumamosi (Oktoba 08), kikosi cha Young Africans kilikuwa kikifanya mazoezi mara moja kwa siku na baada ya kuambulia sare, Kocha Nabi amewafungia kazi wachezaji wake kwa kuwapa Program maalum kuelekea mchezo huo wa marudiano utakaopigwa Jumapili (Oktoba 16) jijini Khartoum, Sudan.
Kikosi cha Young Africans kinatarajia kuondoka kesho Alhamisi (Oktoba 13) kuelekea Khartoum, Sudan kwa ajili ya mchezo huo ambao wanahitaji kupata ushindi wowote ama sare ya 2-2 ili kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Kocha Nabi amesema amerejea uwanjani kwa ajili ya kufanyia kazi mapungufu yao kwa kuelekea kupambania matokeo chanya katika mchezo huo wa marudiano.
Amesema wanaendelea na maandalizi kwa kufanya mazoezi mara mbili kwa siku ambapo asubuhi wanafanya saa mbili na nusu na jioni.
“Tumeona madhaifu yetu katika mechi yetu ya hapa nyumbani, sasa tumeyabeba hayo na kufanyia kazi kuhakikisha tunakisuka kikosi imara kumalizia dakika 90 zilizobakia,” amesema Nabi.