Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Mtibwa akerwa na mapumziko Ligi Kuu

Kondo Mtobwa Kocha wa Mtibwa Habib Kondo

Mon, 2 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mtibwa Sugar bado wanajitafuta kwenye msimu huu, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Habib Kondo akisema licha ya timu hiyo kukaa bila ya kucheza kwa majuma mawili ni tatizo, japo bado haitamuathiri kwa sababu alishaandaa programu za kukabiliana nazo wakati huu.

Kocha Kondo amesema kukaa majuma yote hayo bila ya kucheza michezo ya kiushindani ni pigo kubwa kwao ingawa kutokana na kutambua hilo tangu mwanzoni alishaandaa namna bora ya kuwajenga wachezaji.

“Ni ngumu sana kwa sababu michezo ya kirafiki ambayo tunapata sio ya kiushindani zaidi hivyo kuwafanya hata wachezaji kuchukulia kawaida japo nimekaa nao chini na kufanyia kazi mapungufu yaliyotokea mwanzo,” amesema.

Kondo ameongeza katika kipindi hiki ambacho timu hiyo haichezi amekuwa na jukumu la kutengeneza balansi katika kikosi hicho kuanzia eneo la ulinzi ambalo limeruhusu idadi ya mabao sita katika michezo yao mitatu.

“Tumekosa uwiano mzuri sana hasa kwenye kuruhusu mabao hivyo ni kazi kubwa ambayo tunaifanyia kazi ili kuona ni kwa namna gani tunaweza kuipunguza kama sio kuimaliza kabisa, ila maendeleo ya timu kiujumla ni mazuri.”

Mara ya mwisho kwa Mtibwa kucheza ilikuwa kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Septemba 15, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Kwa sasa timu inajiandaa kwa mchezo wanne wa ligi hiyo itakapoikaribisha Singida Big Stars, mechi itakayopigwa Oktoba 5 kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani Morogoro.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live