Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Morocco mtegoni Geita Gold

Hemmed Morocco Kocha Hemed Morocco

Mon, 20 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Geita Gold imeanza msimu vibaya ikishinda mechi moja tu kati ya tisa za Ligi Kuu hadi sasa na hilo limewafanya viongozi wa timu hiyo kukaa vikao vya mara kwa mara kwa kilichoelezwa kutokuwa na imani na kocha mkuu, Hemed Suleiman ‘Morocco’

Taarifa za kuaminika ambazo tumezipata zinaeleza kocha huyo amekalia kuti kavu huku mchezo ujao dhidi ya JKT Tanzania utakaopigwa Novemba 22 kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita ukimweka zaidi hatarini endapo tu atapoteza na ndio maana kumekuwa na vikao kila mara baina yao.

Hata hivyo, mwenyekiti wa klabu hiyo, Leonard Bugomola alisema vikao vinavyoendelea ni vya kawaida tu na kuhusu kumweka mtu kati kocha huyo kwake halitambui kwani bado wana imani naye kubwa msimu huu.

“Ndio kwanza unanipa hizo habari kwa sababu mimi sina, bado tuna mkataba na kocha wetu Morocco hadi mwisho wa msimu na hatujafanya maamuzi yoyote kuhusu yeye, kama itatokea jambo lolote basi tutatoa taarifa rasmi ila kwa hilo silitambui,”  alisema Bugomola

Wakati Bugomola akiyasema hayo ila watu wa karibu na Morocco waliliambia Mwanaspoti kocha huyo hayuko tayari kuendelea kuifundisha tena kutokana na presha kubwa anayopatiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi.

Hivi karibuni wakati Zahara akiongea na waandishi wa habari, alimtaka kocha huyo kufika ofisini kwake ili kujieleza ni kwa nini timu hiyo inapata matokeo mabovu jambo ambalo kocha huyo alionyesha kukerwa kutokana na maamuzi yaliyofanyika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live