Kocha wa Morocco, Walid Regragui anategemea timu yake kukabiliwa na ugumu kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu nchini Ivory Coast.
Nyota huyo wa zamani wa timu hiyo anaamini ushindani utakuwa mkubwa zaidi pengine kuliko nyakati zilizopita katika historia ya mashindano hayo.
"Kiuhakika litakuwa miongoni mwa mashindano bora katika historia ukiangalia idadi ya wachezaji wa daraja la juu katika kila taifa. Kuna wachezaji wakubwa waliopo katika timu zote ambao wanacheza katika klabu kubwa duniani," alisema Regragui.
Morocco ambayo ilifika hatua ya nusu fainali katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar mwaka jana, ni miongoni mwa nchi zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Afcon mwaka huu ikiwa katika kundi F na timu za DR Congo, Zambia na Tanzania.
Hata hivyo, pamoja na matarajio hayo, Regragui amewataka wachezaji wake kutobweteka na badala yake wanatakiwa waonyeshe ubora wao uwanjani.
"Tuna uhalisia katika kujua kwamba kuna ngazi ya hamasa na ya kwetu ni ya juu. Ninafikiria hili kwa timu nyingine pia. Tuna uvumilivu wa kusema tunamheshimu kila mmoja kwamba sisi sio timu bora zaidi kwenye makaratasi lakini hapana tunataka kupeleka hili taji nyumbani," alisema Regragui.
Hizo ni fainali za kwanza za Afcon kwa Regragui kuiongoza Morocco na hapana shaka atatamani kufanya kile alichokionyesha kwenye Kombe la Dunia 2022.