Yanga ina dakika 90 za kuandika rekodi mpya ya kufuzu hatua ya robo fainali endapo itashinda kesho Jumapili itakapopambana na US Monastir ya Tunisia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, huku kocha wa zamani wa timu hiyo, Hans Pluijm akiwapa akili tya kutoboa Kwa Mkapa.
Yanga itavaana na Monastir katika mechi ya Kundi D, huku kikosi hicho cha Kocha Nasreddine Nabi kinahitaji ushindi ili kufikisha pointi 10, sambamba na kulipa kisasi baada ya kupoteza kwa mabao 2-0 mechi ya kwanza baina yao iliyopigwa Februari 12.
Katika kuiongezea nguvu Yanga ili itoke na ushindi nyumbani, Pluijm anayeinoa kwa sasa Singida Big Stars, alisema amekiangalia kikosi cha timu hiyo na kuona kabisa ina nafasi kubwa ya kushinda nyumbani, lakini ni lazima waingie uwanjani kwa tahadhari kubwa wasijitibulie.
Akizungumza nasi jana, juu ya mchezo huo Pluijm alisema ana matumaini makubwa na kikosi hicho huku akiwataka kuongeza umakini kwenye utumiaji wa nafasi na kujilinda.
"Yanga ina benchi nzuri la ufundi na wachezaji waliopevuka hivyo natambua presha iliyokuwa juu yao kutokana na aina ya mchezo na rekodi wanayotaka kuiandika lakini sina mashaka nao kabisa."
Pluijm aliyewahi kuifundisha Yanga kuanzia mwaka 2014 hadi 2017 aliongeza wachezaji wa Yanga wanahitaji kucheza kwa nidhamu na mtazamo chanya kwa sababu wana timu bora inayojitosheleza.
"Unapoangalia aina ya uchezaji wao unaona ni timu ambayo inaweza kushindania kabisa michuano hii, jambo kubwa ni kujilinda vizuri na kuhakikisha kila nafasi wanayopata wanaitumia vizuri."
Mbali na kuifundisha Yanga ila Pluijm pia amewahi kuinoa Singida United, Azam na sasa Singida Big Stars.
Yanga iliyoko Kundi D la michuano hii iko nafasi ya pili na pointi saba na endapo itashinda italingana pointi na vinara US Monastir wenye 10 huku TP Mazembe ikiwa ya tatu na pointi tatu. Real Bamako ya Mali iko mkiani mwa msimamo baada ya kufikisha pointi mbili baada ya kila timu kucheza michezo minne.