Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Mfaransa aivusha Yanga nusu fainali

Yanga Tano Pacome Maxi 191929 Kocha Mfaransa aivusha Yanga nusu fainali

Thu, 14 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Huko kimataifa Yanga inaogopwa na ukitaka kujua hilo msikie Kocha Mkuu wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Julien Chevalier alichokisema baada ya droo ya mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiwatabiria mabingwa hao wa Tanzania kwenda nusu fainali mbele ya Mamelodi Sundowns kwa sababu kuu moja.

Asec ilioongoza Kundi B, lililokuwa pia na Simba imepangwa kukutana na Esperance ya Tunisia katika mechi hizo za robo fainali zitakazopigwa mwishoni mwa mwezi huu, jambo lililoelezwa na kocha Chevalier kuwa ni ahueni kwa timu hiyo, tofauti na kama ingepangwa na Yanga aliyoitaja kama moja ya timu aliyokuwa akiiogopa kukutana nao.

Kocha huyo, amesema kati ya vitu ambavyo alikuwa anahofia wakati inachezeshwa droo ya mechi hizo za robo pale jijini Cairo, Misri ilikuwa ni kupangwa na Yanga aliodai ipo vizuri sana ndani ya misimu miwili mfululizo.

Amesema licha ya Yanga kupangiwa mpinzani mgumu mwenye ubora mkubwa Afrika, Mamelodi Sundowns lakini kama ikijipanga vyema hasa kwa mchezo wa kwanza nyumbani inaweza kufanya kitu cha kushtua katika soka la Afrika kama ilivyofanya msimu uliopita ilipofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika bila kutarajiwa.

"Nilifurahi kuona sijapangwa na Yanga, ndani ya kikosi cha wababe hao wa Tanzania kuna wachezaji niliowafundisha msimu uliopita akiwemo Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki na Yao Kouassi, nafahamu uwezo wao, nje na hao kwa ujumla kikosi chao kipo vizuri," amesema kocha huyo Mfaransa na kuongeza;.

"Ukiondoa hilo msimu uliopita Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ingekuwa timu mbaya isingefikia hatua hiyo, naamini Yanga ina nafasi ya kutinga nusu fainali licha ya kupangiwa Mamelodi Sundowns, inayoonekana kuwa tishio."

Kocha Chevalier amefafanua zaidi; "Yanga inacheza kwa ubora mkubwa iwe nyumbani au ugenini wakati Asec kwa sasa imebomoka safu ya ushambuliaji, hivyo kama tungekutana nao safari yetu ingekuwa fupi mno."

Hata hivyo, kwa mujibu wa ratiba ya mechi za nusu fainali, mshindi wa mchezo kati ya Yanga na Mamelodi atavaana na yule wa pambano la Asec Mimosas dhidi ya Esperance, hivyo kama zote zitavuka basi hatakuwa na ujanja wa kukiepuka kikombe kutegemana na matokeo ya kila mmoja kwenye mechi hizo za robo fainali.

Akiizungumzia Esperance aliyopangwa nayo, amesema amejipanga vizuri kupambana nayo na anaiona nafuu kubwa ya kupata matokeo kutokana na kiwango cha kikosi chake.

"Timu za Afrika Kaskazini zina nafuu kwa kuwa una nafasi ya kutengeneza ushindi mkubwa ukiwa nyumbani kwa kuwa ugenini huwa wanakuja kucheza kwa asilimia 50-60," alisema kocha huyo.

Licha ya Chevalier kuitabiria Yanga kwenda nusu fainali na kuchekelea kutokutana nayo kwenye hatua hiyo ya robo, lakini ukweli ni kwamba Yanga inaonekana kuwa na kibarua kizito mbele ya Mamelodi inayoshikilia taji ya Ligi ya Afrika (African Football League) kutokana na rekodi za wababe hao wa Sauzi kutisha kwa sasa.

Timu hizo zitakutana kwa mara ya pili baada ya awali kucheza mechi za raundi ya pili katika msimu wa 2001 na Yanga kufungwa 3-2 ugenini kabla ya kutoka sare ya 3-3 nyumbani na safari hii Vijana wa Miguel Gamondi wataanza kuwa kuikaribisha Mamalodi Kwa Mkapa kati ya Machi 29-30 kisha kurudiana nao Afrika Kusini Aprili 5-6.

Chanzo: Mwanaspoti