Kocha Mkuu wa Mbeya City, Abdallah Mubiru amesema kuwa ataitumia michezo mitatu iliyosalia ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Mbeya City wanashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa wameshuka uwanjani mara 27 na wamebakisha michezo mitatu kukamilisha msimu wa mwaka 2022/23.
Baada ya kupoteza mchezo uliopita kwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba itakuwa na kazi ya ziada kuikabili Geita Gold kwenye Uwanja wa Nyankumbu Jumamosi (Mei 06).
Kocha Abdallah Mubiru amesema kuwa anawaheshimu Geita Gold na anajua wana timu nzuri yenye ushindani lakini hawatakubali kupoteza michezo miwili mfululizo kwani wakifanya hivyo watazidi kushuka katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
“Tumeumizwa na matokeo yaliyopita yametuonesha tulikosea wapi, tayari tumeufanyia kazi upungufu huo kwa ajili ya kusaka alama ugenini ili tutakaporejea nyumbani tuwe na mtaji mkubwa wa pointi,” amesema Mubiru.
Amesema mzunguko wa pili wa ligi ni mgumu sana kwani umegawanyika katika sehemu kuu mbili, timu zinazo pambania ubingwa na zile zinazopambana kutoshuka daraja hivyo kila mmoja anapigana ili kupata kile anachohitaji.