Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Mbeya City auwakia uongozi, atishia kujitoa

Mubiru Iiiiii Kocha Mbeya City auwakia uongozi, atishia kujitoa

Fri, 13 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mubiru Abdallah, amesema hafurahishwi na mazingira ndani ya kikosi hicho kutokana na kutotimiziwa mahitaji yake, akitishia 'kung'atuka'.

Mbeya City ambayo inajivunia rekodi ya kudumu kwenye Ligi Kuu tangu ilipopanda msimu wa 2013/14, imekuwa ni kati ya timu zenye mashabiki wengi zaidi kwenye ligi kwa miaka ya hivi karibuni.

Msimu huu ilikuwa na mwanzo mzuri huku ikitabiriwa makubwa katika kuzipa upinzani Simba, Yanga na Azam lakini hali imekuwa kinyume cha matarajio ya wengi.

Awali, ilielezwa kuwa tatizo linalowakabili wachezaji ni kutopewa bonasi wanazoahidiwa na mabosi hali iliyowafanya wapoteze morali kwa mechi za karibuni zikiwamo takribani 12 walizokosa matokeo mazuri.

Mubiru aliliambia Mwanaspoti kuwa kwa sasa hafurahii mazingira kwani hata kwenye mapendekezo aliyohitaji hakuna utekelezaji wowote bali kila mtu anafanya lake analotaka.

Alisema katika kipindi hiki cha dirisha dogo amependekeza usajili wa wachezaji saba, lakini hadi sasa ameshangazwa hakuna dalili za utekelezaji huku ishu ya matokeo mabovu akitupiwa lawama yeye.

"Hao unaowaona wamekuja majaribioni sina taarifa nao, mimi nilipeleka ripoti lakini hakuna kilichofanyika, sasa nifanyeje, Mungu ndiye anajua kama msimu utaisha niko hapa," alisema kocha huyo Mganda.

Aliongeza kuwa kikosi alichonacho hakina ubora wa kuweza kuleta ushindani kwenye ligi akibainisha kuwa wapo wachezaji alitaka watolewe kwa mkopo lakini hakuna kilichofanyika.

"Hiki siyo kituo cha michezo (akademi) kwamba nianze kufundisha, nahitaji wachezaji imara wa kuelekezwa kufanya kazi, kwa ujumla nilichotarajia siyo kinachotokea," alisema.

Katika mazoezi ya juzi yaliyofanyika kwenye uwanja wao uliopo Isyesye, ilishuhudiwa baadhi ya sura mpya akiwamo beki wa kati, Juma Ally Babjey.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Joseph Mlundi, alisema Mbeya City siyo ya mtu binafsi kujiamulia, isipokuwa ina utaratibu wake hususani katika masuala ya fedha kwenye utekelezaji.

"Hii ni timu ya Halmashauri inategemea bajeti kutoka huko, siyo mtu mmoja kujiamulia, lakini niseme kwamba ripoti ya kocha tuliipokea tunaifanyia kazi na tayari tumeanza usajili kwa kumleta James Msuva kutoka Singida Big Stars.

"Tunatarajia kabla ya dirisha kufungwa tutakuwa tumemaliza, hakuna anayetaka timu isifanikiwe, kocha atuvumilie hata sisi hatujalala," alisema Mlundi.

Chanzo: Mwanaspoti