Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Mbeya City ainyooshea kidole safu ya ushambuliaji

Mbeya City FC.jpeg Kocha Mbeya City ainyooshea kidole safu ya ushambuliaji

Wed, 1 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Matokeo ya ushindi katika mchezo uliopita dhidi ya Polisi Tanzania yamepunguza presha kwa Mbeya City, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Mubiru Abdalah akisema bado straika wake wanakosa umakini kumalizia mipira ya mwisho.

City ikicheza ugenini katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha iliwalaza Maafande hao bao 1-0 na kuendelea kubaki nafasi yao ya 10 kwa pointi 27, huku wapinzani wakiwa nafasi mbili za mwisho kwa alama 19.

Kwa sasa ligi kuu itasimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC), ambapo timu hiyo itawafuata Kagera Sugar kusaka nafasi ya kufuzu robo fainali, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Machi 5.

Hata hivyo, ligi kuu itarejea tena Machi 10, ambapo City watakuwa nyumbani kuwakaribisha vibonde wa michuano hiyo, Ruvu Shooting huku kila timu ikihitaji ushindi ili kujiweka pazuri.

Mubiru alisema pamoja na ushindi walioupata juzi lakini bado kuna makosa katika eneo la straika kwa kukosa umakini kutumia nafasi kufunga mabao akiahidi kuendelea kulifanyia kazi.

Alisema kwa sasa hesabu na akili zinaelekezwa kwenye mchezo ujao wa kombe la shirikisho, (ASFC) dhidi ya Kagera Sugar akisisitiza kuwa wanahitaji kufuzu hatua inayofuata na kwamba watakuwa makini kupata ushindi.

“Tunashukuru matokeo ya juzi yameturejesha kwenye morali japokuwa bado kazi ni ngumu, upo upungufu kwa vijana haswa eneo la straika kutotumia nafasi wanazopata, tunaenda kujipanga upya na mechi zinazofuata,” alisema Mubiru.

Kocha huyo alisema wanafahamu ugumu katika mchezo huo, lakini watapambana kadri ya uwezo kuhakikisha msimu huu wanafika fainali ya michuano hiyo na kutwaa kombe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live