Kocha wa Mbeya City Abdallah Mubiru amethibitisha kuachana na timu hiyo baada ya kushuka daraja, huku akitaja sababu mbili zilizochangia matokeo hayo.
Mubiru alisaini kandarasi ya miaka miwili, ambapo kulikuwa na kipengele cha kuongeza mkataba iwapo watabaki ligi kuu na kuvunjika kama timu itashuka daraja na matokeo ndivyo kama ulivyosikia na kuona.
Mbeya City ilishuka daraja kupitia play off baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya Mashujaa ya Championship na kuungana na Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zilizoshuka mapema baada ya kumaliza ligi nafasi mbili za mwisho.
Mubiru raia wa Uganda alisema kutokana na mkataba ulivyokuwa kwa sasa yuko huru, huku akieleza kuwa sababu ya kushuka timu hiyo ni kikosi dhaifu na kwamba alikosa watu aliohitaji akiwamo kipa, beki wa kushoto na straika baada ya Paul Nonga kustaafu.
Pia alisema City ilifanyiwa hujuma za wazi kuanzia mchezo dhidi ya Yanga, KMC na zile za play off (mtoano) na Mashujaa hali ambayo iliwapa wakati mgumu na kwamba kwa sasa anaenda kwao kupumzika kusubiri ofa mpya popote.
“Hata angekuwa Pep Guadiola kwa kikosi changu asingetoboa, wachezaji hawakuwa na kiwango, lakini niliomba kupata kipa, beki wa kushoto na straika wa kusaidiana na Tariq Seif sikupata. Tulidhulumiwa pia baadhi ya mechi,” alisema Mubiru.
Kocha huyo alisema wakati anaenda mapumziko hakufurahishwa na tukio la kupigwa ngumi na mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la Mashujaa na kwamba haelewi dhamira ilikuwa ni nini.
Alisema anashukuru kwa sasa hali yake inaendelea vyema baada ya matibabu hospitali akibainisha kuwa kiongozi huyo alimtafuta mara ya kwanza akamkwepa kabla ya kumrudia tena na kumpiga.
“Mimi simjui na dhamira yake sielewi ilikuwa nini. Alianza kunitafuta nikamkwepa mara ya kwanza, lakini alirudi akanipiga akavunja miwani ikanijeruhi na nimetoka hospitali naendelea vizuri,” alisema kocha huyo aisye na maneno mengi.
Mwenyekiti wa Mbeya City, Joseph Mlundi alisema wanasubiri kikao cha viongozi wa mkoa ili kujadili tathmini ya ligi kwa ujumla na maazimio na kuja na tamko la kulaani tukio la kocha kupigwa.
“Kujua tutabaki na kocha au kuachana naye haijajulikana tunasubiri kikao cha uongozi wa juu, lakini nadhani tutakuja na taarifa rasmi la kulaani tukio hilo ambalo si la kiungwana,” alisema Mlundi.