Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, ameishangaa Ihefu FC kwa kutofunga mabao mengi katika mechi ya juzi kutokana na makosa lukuki waliyoyafanya.
Akizungumza baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Highland, Mbarali mkoani Mbeya, Maxime alisema wamepoteza mechi hiyo kwa bao 1-0 kwa sababu moja tu kwamba hawakucheza vizuri na wamefanya makosa mengi.
Alisema kwa makosa waliyoyafanya walitakiwa wafungwe mabao mengi sana, lakini wapinzani wao, Ihefu wameshindwa kutumia udhaifu wao.
"Niwape pole wachezaji wangu, niwapongeze Ihefu kwa ushindi, lakini nashangaa kwa kutotufunga mabao mengi, hatukucheza mchezo mzuri, tulikuwa na mapungufu mengi sana, sitakiwa kusema maneno mengi, lakini Ihefu FC wamefaidika na makosa yetu," alisema Maxime.
Zipo taarifa kuwa Kagera Sugar walitua Mbarali usiku wakitokea Kigoma kwa basi, siku moja kabla ya kuamkia mechi hiyo, hivyo wachezaji wa timu hiyo walionekana wachovu.
Kocha Mkuu wa Ihefu, Zuberi Katwila, alisema kuwa Kagera Sugar hawakucheza vibaya na waliutawala mpira kipindi chote cha kwanza, ndiyo maana akalazimika kubadilisha mfumo baada ya mapumziko.
"Wenzetu walionekana kuja kwa kushambulia kwenye mechi ya leo na si kuzuia, ikabidi kipindi cha pili tukabadilisha 'plani' iliyozaa bao, kusema kweli ilikuwa mechi nzuri na nguku, Kagera Sugar siyo timu ya mchezo, kuifunga si jambo rahisi," alisema Katwila.
Ni mechi ya kwanza kwa Ihefu kushinda msimu huu baada ya kupoteza nyumbani bao 1-0 Jumanne iliyopita dhidi ya Geita Gold hivyo kuwa na pointi tatu mpaka sasa, huku Kagera Sugar ikipoteza mechi ya pili mfululizo baada ya Jumatano iliyopita kutwangwa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa FC na kutovuna pointi yoyote mpaka sasa.