Kocha Mkuu wa Marumo Gallants, Dylan Kerr amemtolea uvivu straika wake Ranga Chivaviro kwa kukosa baadhi ya nafasi muhimu za kufunga mabao alizopata dhidi ya timu ya Yanga katika Dimba la Mkapa jana Jumatano, Mei 10, 2023.
Katika mchezo huo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Yanga ambao pia ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara waliibuka na ushindi wa bao 2-0 huku Chivaviro akikosa nafasi nne za wazi za kufunga.
Marumo walionyesha mchezo mzuri tena bila woga licha ya kuwa ugenini huku wakiongoza kumiliki mpira na kufanya mashambulizi mara kwa mara kwenye lango la kipa Djigui Diarra.
Baada ya mchezo huo kumalizika, Kerr alisema kuwa walikuwa na nafasi ya kupata zaidi ya mabao mawili hasa kutoka kwa Chivaviro ambaye anafukuzia kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora wa mashindano hayo lakini alishindwa kufanya hivyo na kuiangusha timu yake.
“Umaliziaji ndio kitu muhimu kwenye soka kwani ndicho kinachozalisha mabao, lakini cha kushangaza wakati tulipopata nafasi hatukuzitumia ipasavyo. Tumepata presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa Yanga ambao waliokuwa na vibe mwanzo mpaka mwisho.
“Walipata mpira wa kushitukiza wakatufanyia shambulizi lililozaa bao lao la kwanza, tukaona bao moja sio shida tunaweza kupambana tukarejesha, wakati tukipambana wakapata nafasi nyingine wakafunga bao la pili wakamaliza mechi.
“Hii inatokea kwenye soka, hatuwezi kukata tamaa kwa sababu tumecheza mechi nzuri. Hii pia ilitokea wakati tukicheza na Misri na Pyramids, tulipata nafasi nne lakini tulipata bao moja tu. Leo tumashindwa kupata matokeo kwenye timu bora ambayo ina mchezaji anayefukuzia kiatu cha ufungaji bora wa mashindano haya (Mayele).
“Siwezi kuwalaumu wachezaji wangu, wamejituma, wametumia nguvu nyingi lakini ninachoweza kulaumu ni kutofanya kile ambacho huwa tunakifanya mara kwa mara Afrika Kusini.
“Hatuna straika ambaye anaweza kufunga mabao 20 mpaka 25 kwa msimu kama wanavyofanya akina Erling Haaland, hao ndio washambuliaji tunaowahitaji kwenye kikosa chao.
Marumo ‘Bahlabane Ba Ntwaa’ watakutana tena na Yanga kwenye mchezo wa pili Mei 17, katika Dimba la Royal Bafokeng, wataweza kupindua matokeo mbele ya Wananchi wa Jangwani wenye njaa ya ubingwa wa CAFCC mwaka huu?