Kocha Mkuu wa Inter Miami, Gerardo Martino amesema anahofia mchezaji huyo kuchezewa faulo nyingi kwenye Ligi Kuu ya Soka nchini Marekani msimu huu.
Nahodha huyo wa Argentina sio tu aliifungia mabao mawili timu yake kwenye ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Oralando City, lakini alikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa mabeki wa timu hiyo.
Messi alisukumwa, kuzingirwa na kutishwa kwenye mechi hiyo, madhambi yaliyoonekana wazi yana lengo la kumuumiza nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 na ambayo amekuwa akikumbana nayo kwa zaidi ya miongo miwili kwenye maisha yake ya soka.
“Kama ambavyo Barcelona wanapocheza na Real Madrid au River Plate wanavyocheza na Boca, ndivyo ilivyotokea kwa Messi,” alisema Martino.
“Tulikabiliana na mpinzani mgumu, ilikuwa mechi yenye uhitaji sana.”
Messi alifunga bao la utangulizi dakika ya saba na mambo yalianza kubadilika kadiri kipindi cha kwanza kilivyokuwa kinaendelea hasa baada ya Orlando kukaa nyuma muda mwingi.
Tukio la kwanza lilikuwa dakika ya 19 baada ya Wilder Cartagena kuunawa mpira, Messi alimsukuma kiungo huyo wa Orlando huku akijaribu kuchukua mpira na kupiga adhabu ndogo haraka.
Sekunde 60 baadaye, Messi alikuwa mchezaji wa kwanza kuoneshwa kadi ya njano baada ya kumkwatua kwa nyuma Cartagena.
Mwishoni mwa kipindi cha kwanza mwamuzi Ivan Cisneros alishindwa kupuliza filimbi baada ya kiungo
Sergio Busquets kufanya madhambi ya wazi kwa Josef Martinez.
Wachezaji wa Orlando walionekana kukasirishwa baada ya Messi kumpiga kiwiko Cesar Araujo, madhambi yaliyoonekana kumchukiza kocha Oscar Pareja na aliyeamini nahodha huyo wa timu ya taifa ya Argentina alipaswa kuoneshwa kadi nyekundu.