Kichapo ilichokipata Ihefu FC mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Mashujaa FC kimeonekana kumchanganya akili kocha wa timu hiyo, Zuberi Katwila huku akikiri mabeki wake kufanya makosa ya kizembe akiahidi kukaa nao kufanyia marekebisho kabla ya kuivaa Young Africans.
Ihefu ikicheza dhidi ya Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, ilikubali kuchapo cha mabao 2-0 ikiwa ni kipigo cha pili katika michezo mitatu kwenye Ligi Kuu hadi sasa.
Timu hiyo inatarajia kushuka tena uwanjani Oktoba 4 kuikaribisha Young Africans katika Uwanja wa Highland Estate wilayani Mbarali mkoani Mbeya ukiwa wa raundi ya nne kwenye Ligi Kuu.
Matokeo hayo yaliifanya Mashujaa FC kukaa kileleni kwa muda ikifikisha pointi saba baada ya mechi tatu ikiziacha Young Africans iliyopo nafasi ya pili, Azam FC na Simba SC zenye alama sita na michezo miwili kila mmoja.
Katwila amesema katika mchezo huo pamoja na timu kupambana, lakini mabeki wake walionesha udhaifu kwa kuruhusu mabao mepesi dhidi ya wapinzani wao.
Katwila amesema mabeki walifanya makosa ya kizembe hivyo, watarejea uwanja wa mazoezi kuhakikisha anatengeneza upya kikosi hicho ili mchezo ujao dhidi ya Young Africans waweze kushinda.