Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Ihefu: Tatizo letu tulijiamini kupita kiasi

Katwila.png Kocha Ihefu: Tatizo letu tulijiamini kupita kiasi

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kipigo cha bao 1-0 ilichopewa Ihefu kutoka kwa KMC ikiwa ni siku chache tu tangu iizime Yanga, kimemfanya kocha mkuu wa timu hiyo ya jijini Mbeya, Zubery Katwila kuwatupia lawama wachezaji akisema walijiamini kupita kiasi na kuwapa faida wenyeji kupata ushindi huo kwenye Uwanja wa Uhuru.

Ihefu ilivaana na KMC ikiwa imetoka kuifunga Yanga kwa mabao 2-1 ikirudia ilichokifanya msimu uliopita na Katwila alisema ushindi huo ulichangia kuwafanya wachezaji wa timu hiyo kushuka kwenye Uwanja wa Uhuru wakiwa wanajiamini kupita kiasi na kupoteza kizembe mchezo huo wa Ligi Kuu Bara.

“Tulijiamini kupitiliza lakini ndio mchezo wa mpira wa miguu ulivyo kwani kuna muda unapata kile ambacho hukukitarajia, tumekubaliana na matokeo hivyo tunarudi kujipanga tena upya kwenye michezo ijayo,” alisema.

Katwila aliongeza mbali na hilo ila hata rekodi zao msimu huu kwenye michezo ya ugenini sio nzuri hivyo ni kazi kubwa atakayokabiliana nayo katika kipindi cha wiki mbili kabla ya kukutana na Coastal Union Oktoba 26.

Kichapo hicho ni mwendelezo wa rekodi mbovu kwa Ihefu ikiwa haijawahi kuifunga KMC kwenye Uwanja wa Uhuru kwani mchezo wa juzi ulikuwa ni wa tatu tangu msimu wa 2020/2021 ambapo mara zote walizokutana imepoteza.

Katika michezo mitano ambayo Ihefu imecheza hadi sasa msimu huu tayari imepoteza mitatu baada ya kufungwa 1-0 dhidi ya Geita Gold, (2-0) na Mashujaa na (1-0) na KMC hivyo kuiacha katika nafasi ya nane kwenye msimamo ikiwa na pointi sita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live