Kocha Mkuu wa zamani wa timu ya Taifa ya soka ya Hispania (Wanawake), Jorge Vilda anachunguzwa kama sehemu ya kesi dhidi ya aliyekuwa Rais wa Shirikisho la soka la Hispania Luis Rubiales.
Vilda alifukuzwa kazi hivi karibuni wakati malalamiko juu ya kitendo alichokifanya Rubiales kwenye sherehe za ushindi wa Kombe la Dunia la Wanawake mnamo Agosti 20 yakiendelea.
Rubiales alimpiga busu mdomoni mchezaji Jenni Hermoso, jambo ambalo limechukuliwa kama unyanyasaji wa kijinsia sababu mhusika hakuwa ameridhia.
Katika uchunguzi huo Vilda anatuhumiwa kuhusika katika kumpa presha Hermoso, familia yake na marafiki zake ili kumtaka amtetee Rubiales.
Naye Mkurugenzi wa timu ya soka ya Wanaume pamoja na Mkurugenzi wa masoko wa Shirikisho la soka la Hispania(RFEF), nao wanachunguzwa kuhusiana na kesi hiyo.
Vilda anatakiwa kufika kwenye Mahakama ya taifa tarehe 10 Oktoba.