Nchi za Nigeria na Sudan zimewafuta kazi makocha wao kuelekea kwenye michuano ya mataifa huru ya Africa 'AFCON' ambayo inataraji kuanza January 9-6 February 2022 nchini Cameroon.
Nigeria wao kupitia NFF wamemfuta kazi Mjerumani Gernot Rohr na nafasi yake wamemteua mwalimu wa zamani wa Super Eagles Augustine Eguavoen ambaye aliwahi kuinoa kuanzia mwaka 2005 mpaka 2007 kisha kurejea kama mwalimu wa muda mwaka 2010.
Rohr (68) amesema “Inachanganya kwa kweli ,sitaki kupinga lakini sio njia nzuri nadhani. Na matumaini watakuwa na matokeo bora kwenye AFCON kwa sababu wachezaji wapo kwenye hali na muunganiko mzuri”
Mjerumani huyo alianza kuifundisha Super Eagle kuanzia August 2016 huku mkataba wake ulitarajiwa kumalizika mwezi December 2022 huku akifanikiwa kuipeleka Nigeria kwenye kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi na mashindano ya Afcon mwaka 2019 akishika nafasi ya tatu.
Kwa upande mwingine, Chama cha soka nchini Sudan (SFA) kimeachana na Mfaransa Hubert Velud baada ya kufanya vibaya kwenye michuano inayoendelea ya FIFA Arab Cup 2021 ambapo amepoteza kwenye michezo mitatu akiruhusu kufungwa magoli 10 huku yeye akiwa hajafunga hata goli moja na sasa nafasi yake itachukuliwa na mwalimu wa muda Burhan Tia.
Kwenye AFCON wamepangwa kwenye kundi D sambamba na mataifa ya Nigeria, Egypt na Guinea-Bissau huku kibarua chake kikiwa ni kuvuka hatua ya makundi kwenye michuano hiyo.