Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Denis Kitambi amesema timu yake imejipanga vyema kwa ajili ya kuibuka na ushindi katika mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC utakaochezwa leo Alhamis (Mei 09) katika Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Kitambi amesema timu yake imetoka kupoteza mechi mbili mfululizo baada ya kufungwa na JKT Tanzania kwa mabao 2-0 na pia ikatolewa katika Kombe la Shiriklisho ‘CRDBFC’ kwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union.
Amesema matokeo hayo si mazuri kwao, lakini ameahidi kupambana na kushinda michezo yao mitano iliyobakia ya Ligi Kuu ili wabaki katika Ligi Kuu Bara.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Geita Gold FC ipo nafasi ya 13 baada ya kucheza michezo 25. Timu hiyo imeshinda mechi tano, sare tisa na kupoteza mechi 11. Imefunga mabao 16 na kufungwa mabao 28.
Baada ya mchezo na Namungo FC, Geita Gold FC itacheza na Coastal Union Mei 14 katika Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita. Mei 21, Geita Gold FC itacheza na Simba SC katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Mei 25, Geita Gold FC itacheza na Singida Fountain Gate katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na Mei 25, watacheza na Azam FC katika Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita.