Baada ya mwenendo mbaya wa Chelsea katika Ligi Kuu ya Engalnd, taarifa za ndani zinaeleza kwamba bodi ilikukatana kwa kikao cha dharura na kuamua kumpa mechi mbili za mwisho kocha wa timu hiyo, Graham Potter kabla ya kumfungashia virago.
Inaelezwa kikao hicho kilifanyika baada ya Chelsea kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur wikiendi iliyopita ambapo alikuwa amefikisha mechi tatu bila ya kufunga bao hata moja huku ikiwa ni mechi sita bila ushindi.
The Telegraph imebainisha kwamba mechi mbili ambazo bosi huyo amepewa ni dhidi ya Leeds United katika Ligi Kuu England na Borussia Dortmund ule wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na ikiwa atapoteza huenda ukawa mwisho.
Mbali ya kufungwa na Spurs, kipigo ambacho kiliwaumiza mashabiki wengi wa timu hiyo ni kile cha bao 1-0 dhidi ya Southampton iliyopo kwenye mstari wa kushuka daraja.
Chelsea itakutana na Leeds Jumamosi wiki hii kabla ya kukipiga na Dortmund Jumanne wiki ijayo ambapo itahitaji kupindua meza kwa kushinda mabao mawili na kuendelea ili kupenya kwenye hatua inayofuata kwa sababu mechi ya kwanza ilikubali kupokea kichapo cha bao 1-0.
Awali kulikuwa na taarifa kwamba mmiliki wa timu hiyo, Toddy Boehly anaamini itachukua muda kwa usajili wa zaidi ya Pauni 600 milioni alioufanya kuanza kuonyesha matunda, hivyo kumuamini kocha wake.
Kwenye makubaliano ya awali ilikuwa kwamba kocha huyo atapewa timu kwa mpango wa kuijenga kwa muda mrefu kama ilivyokuwa alipokuwa Brighton.
Lakini presha kutoka kwa mashabiki inaonekana kuwa kubwa zaidi kiasi cha kuwafanya wabadilishe mpango licha ya Potter kuwa na mkataba mrefu wa miaka mitano ambao unamwezesha kukunja Pauni 10 milioni kila mwaka.
Hivi sasa hali inaelezwa kuwa sio nzuri baina ya mabosi na wachezaji wa kikosi cha kwanza, huku baadhi wamekuwa wakitaka kocha huyo aendelee na wengine wanasisitiza aondoke.
Kuna wachezaji wanaonekana kuchukizwa kuachwa nje kwenye baadhi ya mechi na baadhi ya michuano ikisababishwa na wingi wa mastaa kikosini.
Mfano kwenye mechi dhidi ya Spurs, supastaa Mateo Kovacic aliikosa mechi hiyo kutokana na ugonjwa uliokuwa unamsumbua wakati Trevoh Chalobah, Marc Cucurella, Carney Chukwuemeka na David Datro Fofana hawakujumuishwa kabisa kikosini kwa sababu idadi ya mastaa wanaotakiwa kuwepo benchi ilitimia.
Hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi na itashuhudiwa wachezaji wengi wenye majina makubwa wakikaa jukwaani ikiwa N’Golo Kante, Christian Pulisic na Edouard Mendy watarudi kutoka kwenye majeraha yanayowasumbua kwa sasa.
Kwa sasa Chelsea inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa imecheza mechi 24 za michuano yote ikikusanya alama 31 baada ya kushinda mechi nane, sare saba na kufungwa tisa.
Akizungumzia uwezekano wa kufungashiwa virago, Potter aliwahi kusema bado anaamini mabosi wa wanamlinda.
“Mmiliki ni bilionea. Ni mtu anayejielewa na makini sana pengine kuliko mimi, hivyo anafahamu changamoto tunazopitia na sehemu ambayo tunahitaji kufika,” alisema Potter.
“Nimekuwa hapa kwa miezi minne (kipindi hicho), lakini wiki tano hadi sita zote hatukuwa na wachezaji muhimu ambao wengi walikuwa kwenye timu zao za taifa. Lengo la kuichukua timu hii ilikuwa ni kuijenga sababu nilifahamu inapitia nyakati ngumu.”