Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Algeria, Chabab Riadhi de Belouizdad ‘CR Belouizdad’, Marcos Paqueta raia wa Brazil amejikuta akiweka wazi mapema kuwa anatarajia mchezo mgumu dhidi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kutokana na ratiba yao kubana.
CR Beluoizdad ambao ni wapinzani wa Young Africans katika ligi ya mabingwa Barani Afrika kutokana na kupangwa pamoja katika kundi D la michuano hiyo pamoja na timu za AI Ahly kutoka Misri na Madeama kutoka Ghana.
Akizungumza baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa USM Alger katika mchezo wa ligi kuu mwishoni mwa juma lililopita, kocha huyo alisema: “Ratiba haijakuwa rafiki kwetu ukitazama hapo mbeleni utaona kuwa tuna michezo mingi migumu mbele yetu lakini bado tumecheza mechi mfululizo.
“Tunakwenda kucheza michezo mingine miwili mbeleni kisha ndio tutakwenda kucheza wa kwanza na Young Africans ambayo ni moja ya timu ngumu Afrika, huo utakuwa ni mchezo wa kimataifa hivyo tulitakiwa kupata muda mwingi wa kujiandaa ili tuweze kufanya vizuri,”alisema kocha huyo.
CR Belouizdad kabla ya kukutana na Young Africans wanatarajiwa kukutana na michezo mingine miwili ya ligi kuu nchini Algeria dhidi ya Paradou FC Novemba 14 kisha Novemba 15 dhidi ya JS Kabylie.
Baada ya hapo CR Belouizdad watacheza mchezo wao dhidi ya Young Africans Novemba 24 wakiwa nyumbani kwao nchini Algeria.