Kocha Mkuu wa Klabu ya Brentford Thomas Frank, anaamini Kai Havertz alipaswa kupewa kadi nyekundu kabla ya kufunga bao la ushindi katika ushindi wa 2-1 wa Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates juzi Jumamosi (Machi 09).
Bao la kichwa la Havertz dakika ya 86 lilihitimisha mechi hiyo kali ambayo Declan Rice alifunga la kwanza kabla ya kipa wa Arsenal Aaron Ramsdale kurudishiwa mpira langoni lakini akafanya makosa na wapinzani kusawazisha.
Ramsdale alianza katika mechi hiyo kutokana na David Raya kutostahili kucheza dhidi ya klabu yake kuu.
Havertz alioneshwa kadi ya njano kwa kumpiga kwa kiwiko Kristoffer Ajer kabla ya kugongana kidogo na Nathan Collins katika dakika ya 66, na hivyo kusababisha ukaguzi wa VAR kwa Penati.
“Hakuna alichopewa na Havertz aliepuka kupata kadi, kwani ni wazi alijidondosha kirahisi. Havertz alijiangusha na ni wazi na wazi,” alisema Frank.
“Hiyo bila shaka ingelikuwa kadi ya pili ya njano na kadi nyekundu. Na kisha hangeweza kufunga bao la ushindi na tunatumaini labda tungepata kasi zaidi, labda kushinda mchezo.”
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alisifu nchango wa Havertz baada ya mchezaji huyo aliyesajiliwa kwa Pauni milioni 67.5 msimu wa majira ya joto kutoka Chelsea kuanza polepole kabla ya kufikia kiwango cha hali ya juu hivi karibuni, akifunga mabao manne na kutoa pasi mbili za mabao katika mechi zake nne zilizopita za Ligi Kuu.
“Kama mtu angeniambia baada ya miezi miwili au mitatu ya kwanza kwamba uwanja mzima utaimba wimbo wake kwa mapenzi hayo, kwa hisia hizo, ingekuwa vigumu kuamini,” alisema Arteta.
“Hicho ndicho kinachotokea kwa watu wazuri. Ni mchezaji wa kipekee.”