Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Azam amrudisha Dube kundini

Rdg Kocha Dabo Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo

Tue, 5 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuna kila namna kwamba Prince Dube ameamua kurudisha majeshi nyuma akajipange upya baada ya kufanya kikao kirefu na kocha wake, Yousouph Dabo.

Sasa ni rasmi atarudi kundini kuelekea mechi za mwisho wa msimu. Dube aliandika barua jana ya kutaka kusitishiwa mkataba wake na Azam lakini akapewa masharti ya kulipa dola 300,000 sawa na Sh700Milioni ambazo zipo kwenye makubaliano ya mkataba wake unaomalizika 2026.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Dabo baada ya kusikia sekeseke hilo amemuita Dube mezani kutaka kujua kuna nini kinaendelea na baada ya majadiliano marefu kwenye ofisi ya kocha huyo kwenye Uwanja wa Azam Complex Dube akakubali kurejea mzigoni na kuachana na ishu yake.

Dabo alipoulizwa na Mwanaspoti alijibu kwamba; "Dube bado ni mchezaji halali wa klabu na ndio maana nikazungumza naye, hayo mengine ni mambo ya ndani."

Katika barua yake, Dube aliomba avunjiwe mkataba lakini asilipe kiasi kilichotajwa kwenye mkataba bali arudishe pesa aliyopewa wakati anasaini mwaka jana ambayo ni dola 200,000 zaidi ya Sh510 milioni.

Lakini jibu alilokutana nalo Dube ni kwamba hakuna mazungumzo mengine yoyote zaidi ya kufuata mkataba unavyotaka. Awali, inadaiwa alitaka kutoa dola 150,000 ambazo ni Sh382 milioni kutoka kwa klabu inayomuwinda kimyakimya.

Habari zinasema kwamba wakurugenzi walishakubaliana kwamba Dube aondoke kutokana na kukerwa na 'kitrendi' chake cha kuandika barua ghafla bila kusema chochote. Walitoka na kauli moja kwamba Dube kaonyesha dharau kubwa na hakuna kingine zaidi ya kumruhusu aondoke ila kwa makubaliano ya kimkataba ambayo ni kulipa dola 300,000.

Baada ya mazungumzo yake na Dabo, Dube atarudi kwenye timu na kuendelea kuitumikia klabu hiyo lakini kwa kifupi ni kwamba harakati zake zimekwama kwa sasa kutokana na mahitaji ya mkataba.

Lakini vyanzo vya ndani kutoka klabu inayotajwa kuwa nyuma ya harakati hizo za Dube, ni kwamba wao wako tayari kutoa nusu ya fedha zilizotajwa lakini wanaogopa kujitokeza hadharani kwa sababu wataonekana walishafanya ushawishi.

Ndiyo maana walimtanguliza Dube mwenyewe mbele ili wamsaidie chini kwa chini. Lakini harakati hizo zinaonekana kuwa ngumu ingawa lolote linaweza kutokea kuelekea mwisho wa msimu huku Azam wakisisitiza kutokuwa na wasiwasi wowote.

Kuna sababu kubwa tatu mpaka nne zinatajwa kama chanzo cha yeye kuomba kuondoka, ikiwemo Yanga, Ihefu na timu za Zimbabwe, lakini vyanzo vya kuaminika vinasema kuna kitu kinaendelea kimyakimya njiapanda ya Jangwani.

YANGA Wanaamini Prince Dube anaweza kuwa mtu sahihi wa kuziba nafasi ya Fiston Mayele. Inaaminika kwamba Yanga wamekuwa wakihangaika kumshawishi mchezaji huyo kwa muda mrefu kutua katika kikosi hicho kutokana na uwezo wake.

Hivi karibuni wakati Azam FC ikiwa mikoani kwa mechi za Ligi Kuu, Dube alionekana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa akishuhudia mechi ya Yanga ambayo ilishinda mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad.

Dube hakusafiri na Azam kwa sababu ni majeruhi ambapo amekosa michezo kadhaa hadi sasa. Nyota huyo hajacheza mechi ya Azam FC tangu Februari 19 alipoingia kipindi cha pili dhidi ya Tabora United. Hakusafiri na timu katika mechi mbili za mikoani - Mbeya dhidi ya

Tanzania Prisons na Mwanza dhidi ya Singida Fountain Gate. Lakini Mwanaspoti linajua kwa kawaida Azam FC husafiri na wachezaji wake hata kama ni majeruhi kama sehemu ya kujenga umoja. Hata hivyo, Dube hakusafiri ikisemekana alikataa kusafiri kama sehemu ya shinikizo ili aachwe huru.

Habari za ndani ni kwamba inasemekana kuna mfanyakazi mmoja wa Yanga ambaye hapo kabla alikuwa Azam ndiye anayechora ramani ya Dube kuhamia Yanga na klabu hiyo ina uhakika kwamba ishu itakwenda kirahisi kwani staa huyo ameshaanza 'kuingia kwenye mfumo'.

IHEFU Inaweza kuwa ajabu lakini bado ni kwa asilimia ndogo. Wamiliki wapya wa Ihefu wanataka kumnasa mchezaji huyo kwa gharama yoyote wakiamini atawasaidia kurahisisha safari ya mafanikio.

Kwa mujibu wa habari za ndani kutoka kwa watu wa karibu na Dube, mabosi wa Ihefu ambao zamani walikuwa wakiimiliki Klabu ya Singida United iliyopanda daraja mwaka 2017, walitaka kumsajili wakati ule sambamba na Tafadzwa Kutinyu.

Lakini Dube alichagua kwenda Afrika Kusini ambako hata hivyo hakufanikiwa na kuamua kurudi Zimbabwe. Lakini sasa wakiwa na timu mpya, mabosi wale wamerejea tena kwa Prince Dube na kuivuruga akili yake kwa 'mzigo mrefu' waliomuwekea mezani. Lakini Yanga bado imemuingia akilini zaidi.

NYUMBANI ZIMBABWE

Habari kutoka Zimbabwe zinasema timu mbili nchini humo zinapigana vikumbo kumrudisha kijana wao. Mwanaspoti linaijua Highlanders FC, timu aliyokulia Dube ambayo kwa sasa ina wamiliki wapya wenye 'mpunga mrefu' ambao wangependa kumrudisha nyota wao huyo kipenzi cha mashabiki wa timu.

Pia klabu ya Yadah FC ambayo hivi karibuni ilinasa saini ya nyota Khama Billiat nayo iko katika harakati za kumnasa Dube. Timu hizo mbili zinaitesa akili ya Dube, lakini Yanga wanazicheki tu.

Lakini taarifa nyingine zinasema Dube anaamini majeraha yanayomuandama pale Chamazi yanatokana na mambo ya nje ya uwanja hivyo anataka kuondoka ili kujiepusha nayo. Mchezaji huyo alijiunga na Azam FC 2020 akitokea Highlanders ya Zimbabwe - timu yake ya utotoni.

Aliyaanza maisha ya Chamazi kwa furaha kubwa kabla hajaumia kwenye mchezo dhidi ya Yanga, Novemba 25, 2020 na tangu hapo hakurudi kuwa Dube wa kabla ya kuumia. Msimu huu pekee ameshakosa mechi zaidi ya tano kutokana na majeraha ambayo hadi sasa yanamuweka nje.

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema Dube ana mkataba nao hadi mwaka 2026 na unapaswa kuheshimiwa.

Hadi sasa Dube amecheza dakika 734 katika jumla ya dakika 1710 za mechi 19 za Azam FC msimu huu. Dakika hizo alizocheza ni katika mechi 12, huku akikosa mechi saba katika mechi 19 za msimu. Kwa kifupi ni kwamba Dube amecheza chini ya nusu ya dakika za jumla kama angecheza mechi zote msimu huu na hii ni kutokana na pancha za hapa na pale ambazo kimsingi zimekuwa zikimuandama katika misimu yote.

Katika dakika hizo 734 za mechi 12 ambazo amecheza amefunga mabao saba na kutoa pasi mbili za mabao. Mkataba wa Dube na Azam FC unatarajiwa kumalizika ifikapo Juni 2026, ikiwa na maana kwamba bado ana misimu miwili na nusu mbele.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live