Kocha msaidizi wa Azam FC, Kally Ongalla amejibu kauli aliyotoa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele Mei 21 katika Uwanja wa Liti kuwa Azam FC inakamia timu za Yanga na Simba pindi zinapokutana.
Mayele aliyasema hayo baada ya kufunga bao lililoipeleka Yanga fainali Kombe la Azam Shirikisho baada ya Azam kutinga fainali ikiitoa Simba SC mkoani Mtwara katika hatua ya nusu fainali kwa mabao 2-1.
Kally amezungumza leo mkoani Tanga kwenye mkutano na waandishi wa habari akizungumzia maandalizi ya fainali yao dhidi ya Yanga kesho Uwanja wa Mkwakwani;
"Kama sisi tunawakamia, je wakicheza na hao wengine huwa inakuwaje? Huwa wanaachiwa?? Kwangu mimi ni kauli ambayo haijakaa vizuri"
Ongalla amesema licha ya kwamba mchezo wa kesho wa fainali baina ya timu yake na Yanga utakuwa na ushindani mkubwa lakini atapata ushindi kwa sababu amewaaanda wachezaji wake katika maeneo yote na timu yake haitishiki kwasababu kwake ni mechi yenye uzito mkubwa.
Hata hivyo amesema katika kikosi chake watakosekana wachezaji wawili ambao walicheza mechi iliyopita na Coastal Union kwa sababu ambazo hawezi kuzitangaza kwenye vyombo vya habari.
"Kwenye mchezo wa kesho watakosekana wachezaji wawili ambao walicheza na Coastal Union juzi lakini siwezi kuwataja hapa na sitatoa sababu za kutokuwepo kwao.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wa Azam FC, Sospeter Bajana amesema akili, maarifa na ufundi wote watauonesha kesho kwasababu ni fainali ya kihistoria kwao na hawatataka kupoteza ubingwa huo.
"Mchezo wa kesho ukimalizika kila mmoja atakwenda nyumbani kupumzika hivyo hatuna sababu ya kutoonesha kwa mashabiki wetu uwezo tulionao" amesema Bajana.
Wakati Benchi la ufundi na wachezaji wa Azam wakizungumza hayo uwanja wa Mkwakwani umefurika watu ambao wamefika kuwashuhudia wachezaji wa timu hizo mbili.