Kipigo cha bao 1-0 ilichokipata Azam FC juzi dhidi ya Ihefu kimemfanya kocha wa kikosi hicho, Dani Cadena kuweka wazi ni suala la saikolojia tu linalowakabili hivyo kusababisha mwenendo mbovu wa matokeo wanayopata.
Azam ilianza msimu vizuri na kutabiriwa kuleta ushindani kwenye mbio za ubingwa ingawa hali imekuwa ni ya tofauti kwani katika michezo yake mitano iliyopita imeshinda mmoja, sare mmoja na kuchezea vichapo mitatu.
“Tunahitaji kuonyesha zaidi ya hiki kinachotokea kwa sasa hivi lakini kuna muda wachezaji wanaona kama vile msimu umeisha na hakuna cha kushindania tena jambo ambalo sio sahihi na ni la kupambana nalo kisaikolojia.”