Kocha wa Azam FC, Dani Cadena, amesema timu yake ina udhaifu mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji, hivyo anahitaji kufanya marekebisho makubwa eneo hilo sambamba na safu ya ulinzi kabla ya kuivaa Simba Februari 21.
Akizungumza na Mwanaspoti, Cadena alisema baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM walioshinda bao 1-0 amebaini anahitaji kufanya marekebisho makubwa kabla ya mchezo wao wa Jumanne dhidi ya Simba huku akitaja ni mchezo wa kisasi.
“Hatukuwa katika ubora kwenye safu ya ushambuliaji na ulinzi, ni mambo ya kiufundi na nimeandaa programu ya kuhakikisha tatizo hili nalitatua kwa wakati ili kuhakikisha mchezo ujao unakuwa bora na wa ushindani,” alisema Cadena.
Alisema katika soka la sasa ni lazima kuwe na uwiano katika timu kuanzia nyuma, katikati mpaka mbele na timu yake kwa kiasi fulani ilikosa uwiano ulio sawa huku akikiri kuwa eneo la kiungo ni bora na limekuwa likifanya kazi yake kwa usahihi.
“Ukiangalia katika mchezo wetu na KMKM washambuliaji walitengenezewa nafasi nyingi lakini walishindwa kutumia japo walifunga bao moja, hawakucheza vizuri eneo la umaliziaji na pia katika mchezo wetu wa ligi na Dodoma Jiji utaona safu yetu ya ulinzi pia haikuwa sawa, ni mambo ambayo nayafanyia kazi kwa haraka,” alisema.
Alisema kuwa baada ya mchezo na KMKM, anaendelea na mikakati yake ya kuiandaa timu kwa ajili ya ligi kuu ya Bara na mpaka kufika Februari 21, siku ambayo tutacheza na Simba kikosi kitakuwa imara.
Cadena alisema marekebisho anayokusudia kufanya hayahitaji kuona wachezaji wanashindwa kufanya kile anachowaelekeza, hata hivyo, kwa kuwa anachotakiwa kufanya ni kujenga muunganiko mzuri katika timu yake huku akikiri kuhitaji mechio nyingine ya kirafiki kabla ya kumvaa myana Simba.