Kocha wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Julien Chevalier ametumia mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga kuwasoma wapinzani wake hao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Baada ya michezo ya timu za taifa, hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajiwa kuanza ambapo Simba itaanza kuvaana na Asec Novemba 25 ambayo wapo kwenye kundi moja.
Chevalier aliiangalia mechi hiyo kwa televisheni Simba ikifungwa mabao 5-1 kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini pamoja na kuizungumzia Simba pia amemtaja Pacome Zouzou na kusema sasa ameanza kurudi kwenye makali yake.
Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Ivory Coast kwa njia ya simu kocha huyo raia wa Ufaransa alisema amekuwa akifuatilia kiwango cha kiungo huyo ambaye alichukua tuzo ya mchezaji bora wa klabu hiyo msimu uliopita na kuona mchezo dhidi ya Simba ndio alianza kuonyesha ubora wake.
“Nimewaona wote wachezaji wangu wa zamani, lakini nimevutiwa sana na Pacome, nimekuwa namfuatilia sana tangu amekuja Tanzania nafikiri kiwango alichoonyesha juzi ndio ameanza kucheza kwa ubora wake ninaoujua, lakini pia nimewatazama Simba ambao ninakutana nao kwenye hatua ya makundi,”alisema Chevalier.
“Ukiacha goli lake la penalti alitakiwa kufunga zaidi kama angekuwa na utulivu, alipata nafasi za mapema lakini hakuwa ametanguliza utulivu niliwahi kuwaambia huyo ni mchezaji mkubwa sana.”
Kuhusu Yao Yao kocha huyo alisema endapo Yanga itakuwa na washambuliaji bora watafunga sana kwa kutumia krosi zake.