Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Adel Amrouche, anajipanga kukata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo ‘CAS’, kupinga maamuzi ya kufungiwa.
Kocha huyo kutoka nchini Algeria alikumbwa na kadhi ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ wakati wa Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ kufuatia kauli tata aliyoitoa kabla ya mchezo wa Tanzania na Morocco.
Hivi karibuni kilifanyika kikao katika kujadili suala la kocha huyo ambapo halikupatiwa mwafaka licha ya kufutiwa faini ya Euro 9200.
Adel Amrouche alifungiwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, malalamiko yaliyowasilishwa na Shirikisho la Soka nchini Morocco ‘RMFF’ dhidi ya Kocha huyo likimlalamikia kwa kauli zake kuwa nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika inaushawishi ndani ya CAF katika kupanga mechi pamoja na waamuzi.
Kufuatia adhabu hiyo, Kamati ya Utendaji ya TFF pia ilimsimamisha kocha huyo na kumteua Hemed Morocco kuwa Kaimu Kocha Mkuu akiisaidiana na Juma Mgunda.