Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha ASEC: Hapo Pacome bado kabisa

Pacome X Al Ahly Pacome Zouzoua.

Sun, 10 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pacome Zouzoua juzi usiku alifunga bao la kusawazisha la Yanga wakati ikitoka sare ya 1-1 na Medeama ya Ghana, lakini likiwa ni bao la pili katika mechi mbili mfululizo kwenye mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kumfanya kocha aliyewahi kumnoa, Julien Chevalier kushindwa kujiuzia na kumwagia sifa.

Chevalier anayeinoa Asec Mimosas aliyokuwa akiitumikia Pacome msimu uliopita kabla ya kutua Yanga, alisema anachokifanya kwa sasa nyota huyo ni asilimia ndogo ya kile alichonacho, kwani ni mchezaji mwenye akili nyingi na uwezo mkubwa, japo alimtaka aongeze utulivu.

Pacome alianza kufunga bao la jioni katika mchezo dhidi ya Al Ahly ya Misri na juzi alirudia tena dhidi ya Medeama yote yakiwa mabao ya kusawazisha na kuiwezesha Yanga kupata pointi mbili kwenye michezo mitatu iliyocheza katika Kundi D, linaloongozwa na watetezi wa taji hilo, Al Ahly.

Akizungumza nasi kwa njia ya simu kutoka Botswana alipo na timu hiyo iliyokuwa aikicheza na Jwaneng Galaxy kwenye mechi ya Kundi B, Kocha Chevalier alisema amekuwa na utaratibu wa kuangalia mechi pindi wanapocheza wachezaji aliowahi kuwanoa bila kujali wameshaondoka kikosini kwa sasa.

Alisema licha ya Pacome kufunga bao juzi, lakini bado kuna vitu vidogo anavyotakiwa kuongeza ili awe bora zaidi kama anavyomjua, huku akisisitiza ni mchezaji wa viwango vya juu ambaye ana uwezo wa kufunga mabao mengi.

“Pacome kwa sasa anahitaji utulivu, kwani akili kubwa ya maamuzi anapokuwa uwanjani anayo ila kukosekana kwa utulivu kunamfanya kuwa na maamuzi yasiyo na matokeo mazuri. Hicho kinachoonyeshwa naye kwa sasa ni sehemu ndogo ya kipaji alichonacho, namjua,” alisema Chevalier na kuongeza;

“Anaweza kufunga mabao hatari na kwa uwezo wake mkubwa anaweza kufanya jambo katika ukuta wowote, nafurahi kuona wachezaji wenzake wa Yanga wameanza kumjulia jinsi ya kucheza naye kwa kumpa pasi za haraka karibu na eneo la wapinzani.

“Jana alipata nafasi mbili kipindi cha pili na akashindwa kuzitumia kwa shida ya utulivu, lakini Yanga inaweza kutinga robo fainali, ina timu nzuri na kundi linatoa matumaini zaidi,”

Yanga iliyorejea nchini, itarudiana na Medeama wiki ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya mechi za makundi kusimama hadi mwakani itakapoikabili CR Belouizdad ya Algeria nyumbani kisha kuifuata Al Ahly, jijini Cairo na kama itakuwa imevuna pointi za kutosha itatinga robo na kuandika historia mpya kwao kwenye ligi hiyo tangu michuano ilipobadilishwa mwaka 1997.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live