Mbali ya kutangaza kuondoka hivi karibuni na kuwaumiza mashabiki wa Liverpool, hatimaye ripoti zinadai Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp yupo mbioni kuipa dili timu hiyo litakalowawezesha kupata Pauni 10 milioni.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Daily Mail, Klopp ataipa Liverpool pesa kupitia kampuni mbalimbali zilizojitokeza kutaka kutengeneza video (makala) ya maisha yake ndani ya timu hiyo kwenye miezi sita ya mwisho.
Kampuni inayopewa nafasi kubwa ya kushinda dili hilo Disney ingawa Netflix pia ilihitaji, kabla ya kujiondoa kwa sababu Liverpool haikuwa tayari kuwapa ruhusa ya kuchukua video kwenye baadhi ya maeneo kama vyumba vya kubadilishia nguo.
Awali dili hilo lilikuwa kwa Sky Sports na TNT Sport, lakini kampuni hizo zilijitoa kwa sababu ya pesa ndefu iliyohitaji Liverpool.
Mabosi wanaamini kuondoka kwa Klopp kutawapa pesa nyingi kupitia dili hilo ingawa mashabiki ndio wanaonekana kuumia.
Inaelezwa moja ya changamoto inazokutana nazo timu hiyo ni kwenye dili hilo ni msimamo wa Klopp, ambaye hataki kampuni hizo kuwafuata wachezaji vyumbani na maeneo mengine ya faragha.
Hata hivyo, mabosi wa Liverpool hawataki kupoteza ofa iliyo mezani kwa sasa na taarifa zinadai wapo kwenye hatua ya mwisho kusaini makubaliano.