Jurgen Klopp anaanza kuzoea maisha bila ya pilikapilika za soka.Mjerumani huyo kwa sasa hana kazi baada ya kuamua kujiweka kando kwenye kazi yake ya ukocha akienda kupumzika baada ya miaka tisa ya kuinoa Liverpool.
Klopp, aliweka wazi kwamba hana haraka ya kurudi kwenye benchi la ufundi na kipindi hiki anatumia mapumziko yake kuwa karibu na mkewe, mrembo Ulla Sandrock.
Na kitu atakachofanya kwa sasa ni kuogelea tu kwenye mabwawa kwenye makazi yake mapya huko Majorca, Hispania. Klopp, 56, alitumia Pauni 3.4 milioni kununua makazi mapya na atatulizana huku kukusanya tena nguvu baada ya kuchoshwa na purukushani za Anfield.
Klopp aliiambia BILD: “Nilikuwa na ndoto za kuja kuishi huku maisha yangu yote. Napenda hali ya hewa ya huku, majira na nawapenda watu wake pia. Kuna mambo mengi, nina marafiki pia huku.”
Licha ya kupendezwa na maisha ya visiwa hivyo vya Balearic, Klopp alifichua kwamba hawezi kuishi Hispania kwa maisha yake yote.
“Siwezi kuwa mhamiaji,” alisema na kuongeza. “Tumekuwa tukija huku nyakati za likizo tangu zamani. Lakini, ninapokuwa hapa, nataka kufanya kila kitu. Nataka kufahamu maisha mapya, sio ya kwenda msituni au kwenye milima.”
Kingine kilichomfanya Klopp kwenda kununua makazi Majorca anakiweka wazi: “Tunazeeka na huduma ya afya hapa ni nzuri sana. Kuna madaktari wengi wa Kijerumani na ningehitaji kufahamu na lugha nyingine pia kwa ufasaha kuweza kupata msaada mambo yanapokuwa mazito.”
Klopp alikiri atakaporejea kwenye kazi ya ukocha hawezi kuwa na nguvu kama awali. Wapo wanaoamini Klopp kakimbia ushindani kutoka kwa Pep Guardiola wa Man City.