Jurgen Klopp amewataka wachezaji wake kusaidiana kuilinda timu isiruhusu mabao hasa katika kipindi hiki ambacho mastaa wao muhimu Mohamed Salah na Sadio Mane wanatumikia timu zao za taifa kwenye fainali za Mataifa Afrika huko Cameroon.
Hofu imetanda huku Klopp akipagawa kwani kikosi chake kimeendelea kupambana bila ya mastaa hao muhimu na tegemeo, na amewasihi wachezaji wake kucheza kwa uangalifu.
Hata hivyo, Liverpool imetinga fainali ya Kombe la Carabao baada ya kuichapa Arsenal mabao 2-0 wiki iliyopita, na itamenyana dhidi ya Chelsea kwenye mchezo huo utakaochezwa Wembley.
Klopp anafahamika zaidi kwa mbinu zake hatari kwenye safu ya ushambuliaji, ameelezea mabadiliko ndani ya kikosi chake na kuwapa onyo wachezaji wake.
“Unapopoteza wachezaji wako muhimu, haimaanishi pia timu haiwezi kupata matokeo mazuri, kwanza unatakwa kuzoea kucheza bila wachezaj wako muhimu, asilimia kubwa ya haya yote ni kucheza bila kuruhusu mabao kizembe, tunatakiwa kujipanga na kucheza kwa uangalifu kwa sasa, nimeona mabeki wetu wamejitahidi kwa jinsi walivyokaba,” alisema Klopp.
Kurejea kwa beki wao kisiki Virgil van Dijk msimu huu imekuwa ahueni kwa Liverpool, hasa baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha ya goti.
Klopp amemtaka Virgil kukubali changamoto ambazo amepitia ili arudi katika kiwango chake bora ambacho kimezoeleka.
“Ilikuwa ni safari ndefu hadi Virgil kupona, amepitia kipindi kigumu, lakini hiyo ni kawaida kwa mchezaji, kwa sasa amerejea baada ya kupona corona na amekosa mechi mbili, nimefurahi kujumuika na sisi tena” aliongeza Klopp.
Klopp anaamini Liverpool itamaliza msimu wa Ligi Kuu England katika nafasi za juu kwenye msimamo na watapambana kupata matokeo mazuri bila ya mastaa hao ambao wana mchango mkubwa Anfield.